"Sumu
Haionjwi!" Huu ndio ujumbe mkuu unaoendelea kutolewa na wananchi
mbalimbali nchini kote, huku wakirejea katika shughuli zao za kila siku kwa
kasi, baada ya kumalizika sherehe za uhuru wa Tanganyika Desemba 9 wakiwa
majumbani.
Leo, Desemba 10,
shughuli za kijamii na kiuchumi hasa sekta ya usafirishaji imeendelea kama
kawaida, huku wito ukitolewa kwa kila mmoja kuhakikisha anaendelea kulinda
amani na usalama wa taifa kwa kushirikiana na serikali.
Katika Kituo cha
mabasi cha Msamvu, Morogoro, ambacho kinahudumia barabara ya Dodoma, Iringa na Dar es salaam
hali ya utulivu na uchangamfu imetawala.
Bilali Yasin
mfanyakazi wa huduma za usafirishaji katika kituo hicho, ameeleza kuridhishwa
kwake na hali ya amani nchini. "Nashukuru Serikali, kuna amani ya kutosha.
Tunaendelea na kazi yetu ya kuhudumia wasafiri," alisema Yasin, akiongeza
kuwa bado wako kazini na huduma za usafirishaji zinaendelea bila vikwazo.
"Tunashukuru nchi kuwa na amani. Tunataka amani hii iendelee,"
alisisitiza.
Ibrahim, abiria
aliyekuwa anaingia kwenye basi kuelekea Dar es Salaam, amesisitiza umuhimu wa
kudhibiti vitisho vyovyote vya kiusalama. "Hali ni shwari (nzuri). Tishio
la kiusalama linapokuwepo lazima lidhibitiwe. Tunaunga mkono namna serikali
inavyodhibiti matukio haya," alisema Ibrahim, akionyesha imani yake katika
jitihada za ulinzi na usalama nchini.
Taarifa kutoka TBC
Morogoro zimeeleza kuwa shughuli zinaendelea kama kawaida Msamvu na wamehimiza
wananchi "wasiogope, kila kitu kinaenda vyema."
Katika jiji la Dar
es Salaam, shughuli za kibiashara na kijamii zimepamba moto, huku wananchi
wakitekeleza majukumu yao bila wasiwasi. Kauli ya "Sumu haionjwi" inatumika
kuwakumbusha watu kuacha matukio yaliyopita na kuendelea na maisha yao ya
kawaida, kwani amani ni rasilimali muhimu ya taifa.
Oktoba 29 na
Desemba 9 zinatajwa kama siku ambazo sasa zimepita, na umuhimu upo katika
kuendeleza maisha ya kawaida.Abiria wanaweza kusafiri kwa uhuru kutoka kituo
kimoja kwenda kingine, ishara tosha ya hali ya utulivu nchini.
Serikali na vyombo
vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya kazi bega kwa bega na wananchi
kuhakikisha amani inalindwa, na kwamba kila mmoja anaweza kutekeleza majukumu
yake kwa uhuru na usalama.

0 Maoni