Watanzania
wameaswa kwa dhati kupuuza taarifa za uchochezi na propaganda zinazopandikizwa
kutoka nje ya nchi kupitia mitandao ya kijamii, kwani taarifa hizo hazilengi
kusaidia maendeleo bali zimejaa nia fiche ya kuleta mgawanyiko, machafuko, na
kudhoofisha uchumi. Wataalamu wa masuala ya jamii na usalama wanasisitiza kuwa
kulinda amani ya taifa ndio msingi wa kulinda haki na maendeleo.
Wataalam wanasema
kuwa watu walio wengi wanaoeneza taarifa za uchochezi wakiwa nje ya nchi
hawafahamu hali halisi ya taifa letu, wala hawajui utamaduni, mila, na utulivu
ambao Watanzania wameujenga kwa miaka zaidi ya 60 tangu kupatikana kwa Uhuru.
Inaelezwa kuwa
taarifa hizo, mara nyingi hupakiwa kwenye hoja ya "uhuru wa maoni,"
lakini lengo lake halisi ni kutengeneza migawanyiko ya kijamii au kisiasa.
Kauli inasisitiza kuwa:
"Hawajui namna
ambavyo amani yetu imekuwa nguzo ya maendeleo, uwekezaji, na mshikamano kati ya
makabila zaidi ya 120."
Kwa sababu hiyo,
watu hao wanapotumia kurasa za mtandaoni kuhamasisha maandamano bila kujali
madhara, wanafanya hivyo bila kuwajibika kwa matokeo. Hawatavuruga biashara
zao, hawatapoteza mali, wala hawatakabiliwa na huzuni ya wale wanaopata hasara
baada ya vurugu.
Watanzania
wamehimizwa kutathmini kila taarifa kwa akili pana na kujiepusha na propaganda
zinazoaminisha kuwa mabadiliko hupatikana kwa fujo na uharibifu. Badala yake,
wanapaswa kulinda misingi ya amani ambayo imekuwa urithi wetu tangu enzi za
waasisi wetu.
Amani si jambo la
kupuuzwa, bali ni mazingira muhimu yanayowezesha shughuli za kila siku
kufanyika: biashara kufunguliwa, wanafunzi kusoma, wagonjwa kutibiwa, na
familia kuishi kwa utulivu.
Vitendo vya
uchochezi, hata vinapoanza kama wito wa "maandamano ya amani," mara
nyingi huishia kuwa uwanja wa watu wachache wasiolitakia mema taifa kuingiza
fujo, kuchoma mali, na kupoteza mwelekeo wa lengo la awali.
"Kwa kuwa
vurugu huathiri kila mtu bila kubagua chama, kabila, wala imani, ni jukumu la
kila Mtanzania kukataa kutumiwa kama chombo cha kuharibu misingi ya
taifa."
Wataalam
wamekumbusha kuwa maoni na malalamiko yanaweza kutolewa kupitia njia rasmi,
majadiliano, na haki za kidemokrasia zinazotambulika kisheria. Hakuna
kilichowahi kujengwa kwa moto na mawe, bali kwa utulivu, hekima, na mazungumzo
yenye nia njema kwa nchi.

0 Maoni