Mbunge wa Peramiho Jenista Mhagama afariki dunia

 

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, ametangaza msiba mzito wa Mbunge wa Peramiho, Jenista Joakim Mhagama, aliyefariki dunia leo Alhamisi, Desemba 11, 2025, jijini Dodoma.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kifo hicho kimelitikisa Bunge pamoja na wananchi wa Jimbo la Peramiho ambako marehemu alikuwa akiendelea kuhudumu.

Kupitia taarifa yake, Spika Zungu ameonesha masikitiko makubwa na kutoa pole kwa wabunge, familia ya marehemu, ndugu, jamaa pamoja na wakazi wa Peramiho.

Amesema kuwa taifa limempoteza kiongozi aliyekuwa na mchango mkubwa katika uongozi na utumishi wa umma, huku akiwataka wote walioguswa na msiba huo kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Jenista Mhagama, ambaye alizaliwa Juni 23, 1967, amewahi kushika nafasi mbalimbali serikalini na bungeni, na alikuwa miongoni mwa viongozi waliotajwa kwa utendaji na ushiriki mkubwa katika masuala ya kitaifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bunge, taratibu za mazishi zinaendelea kuratibiwa kwa ushirikiano na familia ya marehemu, na maelezo ya ziada yataendelea kutolewa kadiri maandalizi yatakavyokamilika.



Chapisha Maoni

0 Maoni