Polisi wasema Taifa limeamka salama

 

Jeshi la Polisi limesema kuwa taifa limeamka salama na hali ya utulivu imetawala katika maeneo mbalimbali ya nchi, hali inayotajwa kuwa matokeo ya ushirikiano unaotolewa na wananchi kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo na Msemaji Mkuu wa Polisi David Misime, Tanzania imeanza siku ikiwa shwari huku utekelezaji wa majukumu ya ulinzi ukiendelea kama kawaida.

Katika maelezo yao, Jeshi la Polisi limebainisha kuwa linaendelea kufanya kazi kwa karibu na vyombo vingine vya ulinzi katika kulinda maisha, mali na usalama wa raia.

Limesisitiza umuhimu wa wananchi kuendeleza desturi ya kufuata sheria na kuzingatia kanuni za kiusalama, ambazo zinapaswa kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja na kwa jamii nzima kwa ujumla.

Taarifa hiyo imeelekeza pia umuhimu wa kukataa na kupuuza taarifa zinazotumiwa kuchochea chuki, uzushi, uongo au vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Wananchi wametakiwa kufuta ujumbe wa aina hiyo endapo watakutana nao mtandaoni na kutowapa nafasi watu wanaojitokeza kwa mashinikizo ya kuhamasisha vurugu au uvunjifu wa sheria.

Jeshi la Polisi limehitimisha kwa kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao halali bila hofu, likisisitiza kuwa nchi inaendelea kuwa salama kutokana na ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Limewatia moyo Watanzania kutanguliza uwajibikaji na kuendelea kulinda amani ambayo imekuwa msingi wa maisha na maendeleo ya taifa.

Chapisha Maoni

0 Maoni