Jamii ya kabila la Wahadzabe inayopatikana pembezoni
mwa Ziwa Eyasi Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha ni miongozi mwa makabila yaliyopo
katika mzunguko wa Jiopaki ya Ngorongoro Lengai. Jamii hii ni wanufaika wa mradi wa makumbusho
mpya ya kijiolojia (Urithi Geopark) iliyopo katika mji wa Karatu.
Nchi ya Tanzania na barani Afrika kwa ujumla zipo
kanuni na taratibu mbalimbali ambazo jamii au makabila hujiwekea kama njia ya
kuenzi na kutunza mila na desturi zao.
Katika kabila la Wahadzabe (Watindiga) kwa wanandoa
(mke na mume) kufanya tendo la ndoa na mtu mwingine nje ya ndoa (Kuchepuka) inatafsiriwa kuwa ni
laana kubwa kwa kabila hilo ambapo mtu anayefanya kosa hilo na ikathibitika
adhabu yake ni kuuwawa na mtu aliyewafumania (aliyewashuhudia) kisha akishatekeleza
mauji anapiga ukunga au yowe ili jamii ikusanyike na wazee wa kimila kutoa taarifa rasmi kwa
jamii kuhusu kitendo hicho ambacho kinatafsiriwa kuwa ni kuleta laana na nuksi
kwenye familia.
Njia inayotumika kuwaua waliochepuka ni kuchomwa na
mishale yenye sumu mwilini Mithili ya mnyama anayewindwa, Mishale inayotumika
ina sumu kali ambayo huenea haraka kwenye mwili wa mwanadamu na kupoteza maisha
ndani ya muda mfupi.
Katika maisha ya mapenzi na ndoa kwa jamii ya wahadzabe
zipo kanuni mbalimbali ambazo wamejiwekea ikiwemo kila mwanaume anayeoa na
mwanamke anayeolewa kuheshimu ndoa yake na kuepuka kwa vyovyote vile kushiriki
tendo la ndoa na mwanamke au mwanaume mwingine.
Baada ya kuoana bibi na bwana harusi hutakiwa kuishi
kwa upendo na jamii hufuatilia ndoa hiyo ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu
miongoni mwao anayefanya tendo la ndoa nje ya mwenza wake, jamii hiyo ipo
makini katika kufuatilia mienendo ya wanandoa ili kuhakikisha kuwa usalama wa
familia unakuwepo katika kipindi chote cha ndoa hiyo.
Mchakato wa kuwaua wanandoa waliochepuka haufanyiki
kwa kukurupuka bali uchunguzi na ufuatiliaji wa kina hufanyika mpaka pale watu
wanaoaminika watakapowashuhudia watuhumiwa wakiwa katika kilele cha ndoa hiyo.
Kwa mujibu wa Kiongozi wa Mila za Wahadzabe Mzee
Shagembe Gambai Jamii hiyo imeweka utaratibu huo wa kuwaua watu wanaochepuka
ili kuimarisha nidhamu za familia, ukoo na jamii kwa ujumla ndio maana hadi
sasa utaratibu huo umezoeleka na kuheshimiwa hivyo ni nadra sana kusikia
mhadzabe akichepuka.
Katika kuhakikisha kuwa kila mmoja anajifunza ubaya
wa kuchepuka zoezi la kuwaua waliofumaniwa hufanyika hadharani likishuhudiwa na
jamii yote ya eneo hilo wakiamini kuwa kitendo hicho kinatoa darasa kwa
wanandoa wengine kuacha tabia hiyo.
Mzee Shagembe anasimulia kuwa Ndoa kwa jamii ya
wahadzabe si suala la kufa na kuzikana laah hashaa, jamii hiyo huruhusu
kuachana na ikitokea hivyo unaruhusiwa kuoa au kuolewa na mtu mwingine hata
kama huyo unayeanza naye uhusiano upya ni mtu wako wa karibu au rafiki wa aliyekuwa
mwenza wako.
Jamii ya Wahadzabe hawaamini katika ndoa za mke
zaidi ya mmoja, Kwao ndoa ya mke na mume mmoja tu na hairuhusiwi mwanaume kuoa
mke zaidi ya mmoja sababu kubwa ikiwa ni kuimarisha upendo kwa wale walioamua
kuishi kama mke na mume.



0 Maoni