Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI
anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila amemtaka Mkandarasi
anayejenga daraja la Mohoro (MAC CONTRACTORS COMPANY LTD) lenye urefu wa mita
100 wilayani Rufiji mkoani Pwani kukamilisha ujenzi wa daraja hilo kwa wakati.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya
ujenzi wa daraja hilo, Mhandisi Mativila amesema fedha za mradi huo zipo hivyo,
amemsisitiza Mhandisi Mshauri anayesimamia mradi huo kumsimamia Mkandarasi
akamilishe kazi hiyo kwa wakati ili kutatua changamoto ya usafiri na
usafirishaji kwa wananchi wa kata ya Mohoro.
"Mliomba fedha kutokana na kazi hii kuongezeka,
Serikali imeongeza fedha 50% ili kazi hii ikamilike, zipo kazi ndogondogo
zinaweza kuendelea kufanyika, hivyo nasisitiza kazi hii ikamilike kwa
wakati", amesema.
Aidha, amewataka Wakandarasi wazawa wajitahidi
kukamilisha miradi kwa wakati ili Serikali iendelee kufanya kazi nyingi na
Wakandarasi wa Kitanzania badala ya kuwatumia Wakandarasi wa nje.
Naye, Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani, Mhandisi
Ibrahim Kibasa amesema ujenzi wa daraja la Mohoro wenye thamani ya Shilingi
Bilioni 17 unatakiwa kukamilika tarehe 24 Machi, 2026 na amemsisitiza
Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wa daraja hilo likamilike kwa wakati ili
wananchi waendelee kupata huduma katika maeneo yao.
"Mradi huu ukikamilika unaenda kuwasaidia wananchi
wa Rufiji, shughuli nyingi za ukanda huu ni kilimo cha mazao mchanganyiko
pamoja na viwanda hivyo kukamilika kwa daraja hili kutaongeza uzalishaji",
amesema.
Kwa upande wake, Mhandisi Mkazi wa mradi huo,
Emmanuel Mahimbo amesema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 50 ambapo
wameshakamilisha ujenzi wa boksi kalavati mbili, nguzo nne na kuinua tuta la
barabara ambapo ameeleza uchelewaji wa kazi umetokana na athari ya mafuriko ya
mwaka jana pamoja na kupitia tena usanifu wa daraja hilo.
Nao, wakazi wa Mohoro, wameeleza furaha yao,
wakisema daraja hilo litawasaidia wakazi wa vijiji vya Mohoro na Chumbi
kusafirisha bidhaa zao, litaepusha vifo
vinavyosababishwa na mamba, litasaidia akina mama kujifungua hospitalini na
kurahisisha usafiri wa watoto kwenda shule.



0 Maoni