Kwa mara ya kwanza nishati mbadala yawa chanzo kikuu cha umeme duniani

 

Kwa mara ya kwanza katika historia, nishati mbadala imeipita makaa ya mawe kama chanzo kikuu cha umeme duniani katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, kwa mujibu wa takwimu mpya kutoka kwa taasisi ya utafiti wa nishati ya kimataifa, Ember.

Ingawa mahitaji ya umeme yanaendelea kuongezeka duniani kote, ongezeko la matumizi ya nishati ya jua na upepo lilikuwa kubwa kiasi cha kukidhi asilimia 100 ya ongezeko hilo la mahitaji, na hata kuchangia kupungua kwa matumizi ya makaa ya mawe na gesi asilia kwa kiasi kidogo.

Hata hivyo, Ember inasema mafanikio hayo yanaficha picha tofauti kimataifa.

Nchi zinazoendelea, hususan China, ndizo zilizoongoza mapinduzi ya nishati safi, huku mataifa tajiri kama Marekani na zile za Umoja wa Ulaya (EU) yakiongeza utegemezi wao kwa vyanzo vya nishati vinavyochangia ongezeko la joto duniani.

Pamoja na mafanikio hayo, makaa ya mawe bado yalibaki kuwa chanzo kikuu cha uzalishaji wa nishati duniani mwaka 2024, nafasi ambayo yameshikilia kwa zaidi ya miaka 50, kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA).

China inaendelea kuongoza kwa kasi katika uwekezaji wa nishati safi, ikiwa imeongeza uwezo wa kuzalisha umeme kwa kutumia jua na upepo kuliko jumla ya uwezo ulioongezwa na mataifa yote mengine duniani.

Hatua hiyo imeiwezesha China kuzalisha nishati mbadala kwa kiwango kikubwa kiasi cha kuzidi ongezeko la mahitaji ya umeme, hali iliyosaidia kupunguza uzalishaji wake wa nishati inayotokana na mafuta ya kisukuku kwa asilimia 2.

Chapisha Maoni

0 Maoni