Bonanza la michezo linaloendelea katika Shamba la
Miti Sao Hill limeendelea kushika kasi na kuleta hamasa kubwa kwa wananchi
kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mufindi na maeneo ya jirani ambapo
bonanza hili limekuwa ni jukwaa muhimu la kuelimisha, kuburudisha, na
kuunganisha jamii katika kampeni endelevu ya kulinda na kuhifadhi misitu.
Michezo hii imeendelea kufanyika jana Oktoba 6, 2025
katika Tarafa ya Nne ya Shamba Mgololo ambapo imeshirikisha timu kutoka vijiji
mbalimbali ambazo ni Lugala, Misitu FC, Mabaoni, Magunguli, Kitasengwa, Mpanga
na Luhunga.
Fainali ya mchezo huu imechezwa kati ya timu ya
Misitu FC na timu ya Luhunga ambapo timu ya Misitu FC imefanikiwa kuibuka na
ushindi wa penati 3 kwa 1 dhidi ya Luhunga baada ya mchezo huo kumalizika bila
kufungana na hivyo kufanya timu ya Misitu FC kuwa mshindi wa jumla kwa upande
wa tarafa ya Nne Mgololo.
Tangu kuanza kwake, michezo mbalimbali imekuwa
ikiendelea kwa ushindani wa hali ya juu kwani timu kutoka vijiji vinavyopakana
na msitu wa Shamba la Miti Sao Hill zimeonesha ari kubwa katika michezo kama
mpira wa miguu, netiboli, kukimbia, kuvuta kamba, mashindano ya kula na kucheza
draft ,na hivyo hali ya ushindani imekuwa ikichochea umoja na upendo baina ya
washiriki huku furaha na shangwe zikitawala uwanjani.
Mbali na burudani, elimu kuhusu matumizi sahihi ya
moto na njia bora za kulinda misitu imekuwa sehemu muhimu ya bonanza hili
na Wahifadhi Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti Sao Hill wameendelea kutoa elimu hiyo kwa
vitendo, wakisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuwa mlinzi wa mazingira.
Hii imekuwa ni fursa adhimu ya kujenga uelewa wa
pamoja kuhusu namna tunavyoweza kutokomeza
matukio ya moto misituni na washiriki na watazamaji wengi wameonesha
kufurahishwa na ubunifu uliotumika katika kuandaa bonanza hili na wengi wamesema kuwa michezo hii si tu
burudani, bali pia ni shule ya maadili, ushirikiano, na uwajibikaji katika
kulinda rasilimali za taifa.
Bonanza limeendelea kuwa darasa la wazi
linalounganisha michezo na elimu ya uhifadhi wa misitu na kadri siku
zinavyosonga, idadi ya washiriki na watazamaji inaongezeka, jambo linaloonesha
jinsi jamii inavyoitikia kwa moyo mmoja kwani watoto, vijana na watu wazima
wamekuwa sehemu ya tukio hili, wakiendeleza ari ya ushiriki na kujifunza mambo
mapya kuhusu utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa misitu.
Bonanza hili linaendelea leo Oktoba 7, 2025 katika
Tarafa ya Pili ya Shamba Ihefu kwa kukutanisha timu mbalimbali zinazolizunguka
shamba katika tarafa hiyo.
0 Maoni