Serikali ya Tanzania imeongeza kasi ya juhudi zake
za kupeleka gesi asilia kwa njia ya bomba moja kwa moja majumbani, ikisisitiza
kuwa mradi huo ndio suluhisho la kudumu la kufanya nishati hiyo kuwa nafuu
zaidi kwa Watanzania.
Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) zimeeleza wazi kuwa lengo kuu si kupunguza bei za mitungi ya
gesi, bali ni kuondoa kabisa hitaji la mitungi hiyo kwa kuwekeza katika
miundombinu ya bomba.
Kauli hiyo inatolewa huku Miradi ya kuunganisha gesi
moja kwa moja majumbani inaendelea. Katika Jiji la Dar es Salaam, kwa mfano,
TPDC inatekeleza mpango wa kuunganisha nyumba zaidi ya 1,000 na mtandao huo.
Juhudi hizi za Serikali za kusambaza gesi zinakwenda
sambamba na ahadi zilizotolewa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya
2020-2025, ambayo inaitaja gesi asilia kama "injini ya maendeleo ya
Tanzania" na chanzo cha nishati safi.
Aidha Katika baadhi ya maeneo kama Lindi, wateja wa
awali wamepata fursa ya kuunganishiwa gesi bure ili kuondoa mzigo wa gharama
kubwa za kuanzisha matumizi ya nishati hiyo.
Kwa mujibu wa Serikali, gesi asilia inayotumika kwa
njia ya bomba huishia kuwa nafuu zaidi kuliko nishati nyingine, huku ikipunguza
uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Hata hivyo, kuelekea uchaguzi mkuu, kumekuwa na
malalamiko mengi katika mitandao ya kijamii na mitaani yanayotaka Serikali
itilie mkazo zaidi kwenye bei ya sasa ya gesi ya mitungi (LPG).
Wananchi wengi wamekuwa wakiomba bei za gesi, hasa
mitungi midogo ya kujaza, ishuke hadi kufikia kiwango cha chini, wakisisitiza
kuwa nchi yenye rasilimali nyingi za gesi haipaswi kuuza nishati hiyo kwa bei
ghali kiasi hicho.
Serikali imesisitiza kuwa matumizi ya ndani yamepewa
kipaumbele, na kiasi kikubwa cha gesi asilia (trilioni 1.3 kati ya futi za
ujazo trilioni 57.54) kimetengwa kwa matumizi ya miaka mingi ijayo, na hivyo
kuahidi mustakabali mwema wa nishati hiyo kwa Watanzania.

0 Maoni