Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) na
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wameendeleza jitihada za kuitangaza
Tanzania kimataifa kupitia ushiriki wao katika maonesho ya utalii (Tourism Road
Show) yanayofanyika nchini Hispania.
Onesho hilo lililoandaliwa na kampuni ya usimamizi
wa safari (DMC) yenye makao makuu yake nchini Tanzania, (Tanganyika Expeditors)
na kufanyika jijini Barecelona oktoba 06, 2025 , limewaleta pamoja wadau
mbalimbali wa sekta ya utalii wakiwemo mawakala wa safari za kitalii pamoja na
wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya jiji hilo.
Kupitia ushiriki huo, NGORONGORO na TANAPA zimepata
fursa kutoa taarifa muhimu za kuwasaidia mawakala wa usafiri kuandaa safari kwa
wageni wanaotaka kutembelea Tanzania kujionea vivutio mbalimbali
vinavyopatikana hifadhi ya Ngorongoro na
Hifadhi za taifa kama vile Serengeti, Manyara, Tarangire na maeneo mengine ya
kipekee yanayosimamiwa na taasisi hizo.
Mbali na NCAA na TANAPA, washiriki wengine kutoka
Tanzania ni pamoja na Miracle Experience -Tanzania, Auram Treks, Karafuu Beach
Resort and Spa na Malia Hotels International.
Maonesho hayo ya Tourism Road Show yaliyoanza leo
tarehe 6 Oktoba yataendelea kufanyika katika majiji mengine ya Hispania,
ikiwemo Madrid na Seville ambapo yanatajiwa kuhitimishwa
tarehe 8 Oktoba, 2025.
0 Maoni