
Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park, iliyopo takribani
kilomita 70 kutoka Jiji la Arusha, imeendelea kung’ara katika kurasa mbalimbali
za habari za utalii duniani baada ya kupokea ugeni mzito wa Miss World China
2021 Bi Jiang Sigi, aliyefika hifadhini hapo leo Oktoba 11, 2025 akiwa
ameambatana na washindi wa tuzo ya Miss Travel kutoka Hong Kong - China, Kenya
na Tanzania.
Ziara hiyo maalum ya siku moja, iliyoratibiwa na
kampuni ya Miss Travel World Beauty Pageant T/A Skyvfree International) chini
ya kampuni mama Goshen Safaris, imelenga kuwapa wageni hao wenye ushawishi
mkubwa katika nchi zao fursa ya kushuhudia vivutio vya utalii vilivyopo
Makuyuni, na Kupitia majukwaa yao ya kimataifa, wageni hao wanatarajiwa
kusaidia kuitangaza kwa kuionesha dunia jinsi Makuyuni Wildlife Park inavyozidi
kuwa kivutio cha Kimataifa cha utalii wa wanyamapori, mandhari na utamaduni wa
asili.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mkurugenzi
Mratibu wa Miss Travel World - Tanzania,
Samweli Mulugu alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za kukuza
utalii wa Tanzania kupitia wageni mashuhuri wenye ushawishi mkubwa katika nchi
zao. Aliongeza kuwa kupitia ugeni huo, Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park
itaendelea kujulikana zaidi katika soko la kimataifa na kuvutia wawekezaji wa
sekta ya utalii.
Aidha, alitoa pongezi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa juhudi zake katika kuendeleza utalii endelevu,
kuhifadhi urithi wa asili, na kulinda tamaduni za jamii jirani.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayesimamia utalii – Kanda ya
Kaskazini, Segoline Tarimo, aliishukuru
kampuni ya Goshen Safaris kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya
Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, katika kutangaza vivutio vya utalii vya nchi yetu kupitia
filamu za Tanzania The Royal Tour na
Amazing Tanzania.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wageni kutoka
ndani na nje ya nchi kutembelea Hifadhi hiyo ili waweze kujionea vivutio
mbalimbali vya utalii.
Wakati wa ziara hiyo, wageni walipata fursa ya
kujionea wanyamapori mbalimbali mubashara wakiwemo tembo, twiga, swalapala,
choroa (oryx), pundamilia na wengine wengi, sambamba na burudani za ngoma za
jadi za Kimasai.
Kutokana na kuvutiwa na mandhari na vivutio vya
hifadhi hiyo, wageni hao walieleza azma yao ya kurejea tena Makuyuni Wildlife
Park kwa ajili ya kufanya utalii wa kupanda vilima (hiking) na kuendelea
kutangaza vivutio vya Tanzania kwa dunia.
Na. Beatus Maganja - Arusha




0 Maoni