Takwimu mpya
za uwekezaji kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA)
zinathibitisha wazi kwamba uchumi wa Tanzania upo katika hali nzuri na thabiti,
zikikanusha vikali madai ya kihuni yanayosambazwa mtandaoni kwamba Benki Kuu
imechapisha na kuingiza fedha nyingi kupita kiasi kwenye mfumo.
Ukweli wa
hali halisi ya kiuchumi nchini Tanzania unajionyesha si kwa maneno bali kwa
matendo ya wawekezaji, ambao akili zao za kiuchumi hazidanganywi.
Katika robo
ya kwanza ya mwaka 2025/2026, miradi mipya 201 yenye thamani ya Dola za
Marekani Bilioni 2.54 imesajiliwa na TISEZA. Miradi hii inatarajiwa kuzalisha
takriban ajira 20,800 kwa Watanzania.
Ongezeko hili
la ghafla na kubwa la uwekezaji si bahati nasibu; ni matokeo ya moja kwa moja
ya sera za kiuchumi zenye mwelekeo wa muda mrefu na mazingira rafiki ya
biashara yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Huu ndio uthibitisho mkuu wa
kimantiki kwamba wawekezaji wanaamini utulivu na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Ni kinyume na mantiki kuwekeza mabilioni katika nchi ambayo uchumi wake
unayumba kwa sababu ya "fedha nyingi zilizochapishwa."
Hoja kwamba
kuna fedha nyingi zimechapishwa na kusambazwa kupita kiasi ingethibitishwa na
mfumuko mkubwa wa bei. Kijadi, fedha za ziada zinazokimbiza bidhaa chache
husababisha kupanda kwa bei kwa kasi kubwa. Hata hivyo, Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) imekuwa ikisimamia kwa makini sera za fedha, na viwango vya mfumuko wa
bei vimeendelea kudhibitiwa, vikibakia ndani ya malengo yaliyowekwa.
Utulivu huu
wa bei unakanusha moja kwa moja madai yoyote ya uwepo wa mzunguko wa fedha usio
wa kawaida au uchapishaji wa noti unaohatarisha uchumi. Wawekezaji hawa
wanaoleta dola za Marekani Bilioni 2.54 hawawezi kuhatarisha mitaji yao katika
uchumi uliojaa mfumuko wa bei usiodhibitiwa.
Mafanikio
haya ya uwekezaji yamegusa sekta mbalimbali. Sekta ya Uzalishaji bidhaa
viwandani ndio inaongoza kwa ukuaji wa asilimia 42, ikifuatiwa na Makazi/nyumba
za biashara (15%) na usafirishaji (14%). Hili linaonesha mabadiliko ya kimfumo
kuelekea uchumi wa viwanda.
Zaidi ya
hayo, TISEZA imebainisha kuwa ushiriki wa wawekezaji wa ndani umeongezeka
kutoka asilimia 27 hadi 35, jambo linaloashiria ukuaji jumuishi unaohakikisha
Watanzania wanachukua nafasi yao katika umiliki wa rasilimali na uzalishaji.
Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs) kama Bagamoyo, Kwala, na Buzwagi yamekuwa
nguzo kuu za kuvutia mitaji hii.
Kutokana na
takwimu zilizopo (na takwimu huwa hazidanganyi) uchumi wa Tanzania unaendeshwa
na msukumo thabiti wa kiutendaji na sio porojo za mitandaoni. Takwimu za TISEZA
za Dola za Marekani Bilioni 2.54 ni ishara tosha kwamba viongozi na wawekezaji
wanatekeleza mikakati yenye tija.
Katika
kipindi ambapo nchi nyingi zinapambana kuvutia mitaji, Tanzania inavuna matunda
ya uongozi ulioimarisha miundombinu na kurahisisha mazingira ya uwekezaji, na
kuufanya mfumo kuwa rahisi, wa wazi, na wenye tija kwa maendeleo ya nchi nzima.
Uwekezaji ndio kielelezo cha kweli cha afya ya uchumi, na kwa sasa, afya ya
Tanzania ni njema.

0 Maoni