Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI
anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila ametembelea na kukagua
mradi wa ujenzi wa barabara ya Chumbi-Kiegele yenye urefu wa Kilomita 1.2 kwa
kiwango cha lami, ambapo ameonesha kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo.
Barabara hiyo inajengwa na TARURA wilayani Rufiji
mkoani Pwani kwa lengo la kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
"Mkandarasi aliyefanya kazi hii RAPCO
CONSTRUCTION amejitahidi kukamilisha
kazi kwa wakati, kwa kweli nimeridhika na utekelezaji wa mradi huu,
nimuombe Mkandarasi aendelee kufanya kazi kwa ubora na kwa wakati kwenye miradi
mingine atakayoweza kuipata ya OR-TAMISEMI kupitia TARURA", amesema.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa
karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana
huku akitoa wito kwa Makandarasi kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kwa
kuzingatia muda uliopangwa.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa TARURA mkoa
wa Pwani, Mhandisi Ibrahim Kibasa amesema mradi huo umegharimu Shilingi Bilioni
1.499 na utekelezaji wake umefikia asilimia 95, huku ukihusisha uwekaji wa
mifereji ya maji ya mvua pamoja na taa za barabarani 18.
"Mkandarasi amejitahidi kufanya kazi vizuri na
amekamilisha kwa wakati, tunaamini ni mtanzania mwenzetu ambaye ametuwakilisha
vizuri kutekeleza mradi huu ambao utasaidia wananchi kuzifikia huduma za
kijamii kiurahisi", amesema.
Wananchi nao wametoa pongezi kwa Serikali kwa
kuwaletea maendeleo yanayoonekana kwani hali katika eneo hilo la Chumbi ilikuwa
mbaya, walikuwa wanashindwa kusafirisha mazao na mifugo yao lakini ujenzi wa
barabara hiyo utarahisisha usafiri, kukuza biashara na kuongeza upatikanaji wa
huduma muhimu kama afya na elimu.



0 Maoni