Ofisi ya Msajili wa Hazina imesisitiza umuhimu wa mashirika ya umma katika kuhakikisha mafanikio ya utalii wa matibabu kwa kuboresha huduma za afya na miundombinu.
Kauli hiyo imetolewa na Bw. David
Shambwe, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji wa Mashirika yasiyo ya Kibiashara,
alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) yaliyofanyika leo, Agosti 15, 2025, katika Ukumbi wa Maktaba,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Bw. Shambwe amesema mashirika ya umma
ni rasilimali za kimkakati kwa maendeleo ya taifa katika sekta ya afya, kwa
kuwa yanatoa huduma maalum na za kiwango cha juu ambazo pengine sekta binafsi
pekee isingeweza kuzitoa.
Ameongeza kuwa mashirika hayo
yamewekeza zaidi katika sekta ya afya, hivyo kuongeza uwezo wa nchi kutoa
huduma za matibabu kwa viwango vya kimataifa.
Ameeleza kuwa Ofisi ya Msajili wa
Hazina imekuwa ikichangia katika kuboresha sekta ya afya kwa kuimarisha ubora
wa huduma, uimara wa kiutendaji na ushindani kwa kuweka misingi ya utawala
bora, uimara wa kifedha, ufanisi wa uendeshaji, na maendeleo ya rasilimali
watu.
Kwa mujibu wa Bw. Shambwe, uwekezaji
na uboreshaji wa miundombinu katika sekta ya afya unaongeza uwezo wa Tanzania
kuhudumia wagonjwa wa ndani na wale wanaotoka nje ya nchi, hali inayochochea
ukuaji wa utalii wa matibabu.
0 Maoni