Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete,
amezitaka nchi za Afrika kuwekeza michango ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya
jamii katika miradi mikubwa ya maendeleo ili kuchochea ustawi wa bara hilo.
Akizungumza jana Julai
10, 2025, katika Mkutano wa 14 wa Kimataifa wa Watunga Sera wa Sekta ya Hifadhi
ya Jamii Barani Afrika unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Arusha (AICC), Mhe. Kikwete alisema mifuko hiyo ina uwezo mkubwa wa kuchangia
maendeleo ya miundombinu kama barabara, reli, bandari na huduma za kijamii kama
afya na elimu.
“Huu ni wakati wa
kuhakikisha kuwa rasilimali hizi tunazozikusanya kutoka kwa wanachama wetu
hazikai tu kwenye mabenki, bali zinafanya kazi na kuleta matokeo chanya katika
maendeleo ya bara letu,” alisema Mhe. Kikwete.
Mkutano huo ulifunguliwa
rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip
Mpango, huku ukiwakutanisha mawaziri, watunga sera na wataalamu wa sekta ya
hifadhi ya jamii kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Kwa mujibu wa Waziri
Ridhiwani, jukwaa hilo linatoa fursa kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu na
kuja na mikakati ya pamoja itakayowezesha mifuko hiyo kufanya uwekezaji wenye
tija.
Kauli mbiu ya mkutano huo
ni: “Mifuko ya Hifadhi ya Jamii: Chachu ya Maendeleo ya Miundombinu na Ukuaji
wa Kiuchumi na Kijamii Barani Afrika.
0 Maoni