Waziri wa Maliasili na
Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, leo Julai 10, 2025, amekutana na kufanya
mazungumzo na Mkurugenzi Msaidizi wa UNESCO anayeshughulikia masuala ya
Utamaduni, Ernesto Ottone, pembezoni mwa Mkutano wa 47 wa Kamati ya Urithi wa
Dunia unaoendelea jijini Paris, Ufaransa.
Katika mazungumzo hayo,
viongozi hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano baina ya UNESCO na Tanzania,
hususan katika uhifadhi wa Maeneo ya Urithi wa Dunia yaliyopo nchini, yakiwemo
hifadhi na maeneo ya kihistoria yanayotambuliwa kimataifa.
Akizungumza baada ya
kikao hicho, Waziri Chana alisema Tanzania ina hazina kubwa ya vivutio vya
utalii na urithi wa kiutamaduni ambavyo vinahitaji kulindwa na kuendelezwa kwa
ushirikiano wa kimataifa.
“Ushirikiano na UNESCO
utasaidia si tu kuhifadhi maeneo haya, bali pia kuyaendeleza kwa manufaa ya
kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Kwa upande wake, Ottone
alieleza dhamira ya UNESCO kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza
shughuli za kiutamaduni, pamoja na kuimarisha juhudi za kuhifadhi vivutio vyake
vya kipekee vinavyovutia ulimwengu.
Kikao hicho pia
kilihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Ali J. Mwadini, pamoja na
wataalam wa masuala ya urithi kutoka Tanzania.
Tanzania ni miongoni mwa
nchi chache barani Afrika zilizo na idadi kubwa ya maeneo yaliyosajiliwa kama
Urithi wa Dunia, yakiwemo Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro na Mji
Mkongwe wa Zanzibar.
0 Maoni