Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania ina
umeme wa kutosha hatua ambayo imechangiwa na kukamilika kwa Miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ukiwemo
Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ambao pekee unazalisha Megawati 2115.
Naibu
Waziri Mkuu ameyasema hayo Julai 10, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua
maendeleo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na
Kinyerezi II ambapo amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na TANESCO yapo
baadhi ya maeneo yalikua na changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini mpaka
sasa yameendelea kuimarika.
Naibu
Waziri Mkuu Dkt. Biteko amefafanua kuwa ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme
unaendana na mahitaji ya ongezeko la watu TANESCO inatarajia kuongeza
uzalishaji umeme katika Kituo cha
Kinyerezi III kutoka megawati 600 katika mpango wa awali hadi kufika Megawati
1000 mpango wa sasa.
‘’Nataka
niseme mbele yenu ndugu zangu, Mhe. Rais
Samia ndio Kinara wa kufanya haya yote yafanikiwe amefanya uwekezaji mkubwa
kwenye Sekta ya Nishati na ndio maana kwenye bajeti iliyopita Wizara hii
imepata Shilingi Trilioni 2.3 kikubwa
anataka wananchi wapate umeme wa uhakika,’’ alisema Dkt. Biteko.
Aidha,
Naibu Waziri Mkuu pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza TANESCO kwa maboresho
makubwa yanayoendelea kufanyika ya kuwahudumia wateja hasa kwa uharaka wao wa
kukabiliana na dharula zozote za umeme zinazojitokeza.
‘’Kuna
maboresho makubwa yamefanyika katika kuwahudumia wananchi naona jitihada kubwa
zinafanyika, mmekuwa na uharaka wa kushughulikia changamoto za umeme lakini pia
niwapongeze kwa kuimarisha Kituo cha miito ya simu sasa wananchi wanahudumiwa
bila gharama yoyote,’’ alisisitiza Dkt. Biteko.
Vilevile,
Dkt. Biteko ametembelea Kituo cha Kupokea Gesi Asilia Kinyerezi kwa ajili ya
kukagua miundombinu ya kusafirisha gesi na kuwataka kuongeza uzalishaji wa gesi
ili kusaidia kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme.
Katika
ziara hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko aliongozana na viongozi mbalimbali akiwemo
katibu Mkuu wa Wizara ya nishati Mha.
Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw.
Lazaro Twange.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni