Serikali
imesema itatoa mafunzo maalumu kwa waandishi wa blogu nchini ili kuwawezesha
kushiriki kikamilifu katika usambazaji wa habari sahihi kuelekea Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2025.
Kauli
hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, katika Mkutano wa Wadau
wa Habari uliofanyika jana Julai 9, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es
Salaam.
Mkutano
huo uliangazia nafasi ya sekta ya habari katika kufanikisha uchaguzi huru na wa
haki, huku hoja ya kuwajengea uwezo mabloga ikitawala mjadala.
Akizungumza
wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama cha Mabloga Tanzania (TBN), Beda
Msimbe, alisema licha ya kuwa baadhi ya mabloga si waandishi wa habari
kitaaluma, wamekuwa wakihusika moja kwa moja katika usambazaji wa taarifa
kupitia majukwaa ya kidijitali.
"Katika dunia ya sasa ya teknolojia na akili
bandia (AI), watu wengi wanategemea taarifa kutoka kwenye blogu na tovuti zaidi
ya mitandao ya kijamii. Ni muhimu mabloga hawa wakapatiwa mafunzo ili kuongeza
weledi hasa katika uandishi wa masuala ya siasa kuelekea uchaguzi mkuu," alisema Msimbe.
Aliongeza
kuwa mabloga wanabeba dhamana kubwa kutokana na idadi yao na nafasi waliyonayo
katika kuunda mitazamo ya wananchi kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa.
Katika
majumuisho yake, Katibu Mkuu Msigwa aliiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) kuandaa mafunzo hayo mapema iwezekanavyo ili kuwaandaa mabloga kwa jukumu
hilo muhimu.
Wadau
mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wameeleza kuwa hatua hiyo ya Serikali ni
ishara ya kutambua rasmi mchango wa mabloga katika mchakato wa kidemokrasia na
maendeleo ya tasnia ya habari nchini.
Kwa
mujibu wa TBN, chama hicho kina wanachama zaidi ya 200 walioko ndani na nje ya
nchi, hivyo mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa na athari chanya kwa upatikanaji wa
taarifa sahihi na zenye kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kipindi cha
uchaguzi na baada ya hapo.
Mkutano
huo ulifunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko,
ambaye alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari na vyombo vya usalama
kushirikiana katika kulinda amani na kuhimiza uvumilivu kuelekea uchaguzi huo.
0 Maoni