Tujikinge na Kipindupindu kwa kutumia Maji Safi na Salama - Dkt. Mmbaga

 

Serikali imetoa rai kwa wananchi kote nchini kuchukua hatua madhubuti za kujikinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko, hasa ugonjwa wa Kipindupindu, kwa kuzingatia kanuni bora za afya ikiwemo matumizi ya maji safi na salama pamoja na matumizi ya vyoo bora. 

Wito huo umetolewa jana Julai 9, 2025 jijini Dar es Salaam na Dkt. Vida Mmbaga, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya, alipokuwa akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali katika kikao kazi cha kitaifa cha Kuhakiki Maeneo Hatarishi ya Kupata Kipindupindu (PAMI’s). 

Kikao hicho kimeratibiwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo ambao umekuwa ukiibuka mara kwa mara katika baadhi ya maeneo nchini. 

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dkt. Mmbaga alieleza kuwa ugonjwa wa Kipindupindu unasababishwa na kinyesi kibichi cha binadamu kinachoingia kwenye maji, na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuchukua tahadhari kwa kutumia vidonge vya kutibu maji, kudumisha usafi wa mazingira na kutumia vyoo bora. 

“Sisi kama Serikali, kupitia kikao hiki, tunakusudia kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia Kipindupindu hasa katika maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa mara kwa mara na mlipuko wa ugonjwa huu,” alisema Dkt. Mmbaga. 

Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa vidonge vya kutibu maji kwa wananchi kwa lengo la kuimarisha kinga dhidi ya maambukizi, sambamba na kuunga mkono mkakati wa kimataifa wa kutokomeza Kipindupindu ifikapo mwaka 2030. 

“Mpango wetu ni kuhakikisha tunatokomeza Kipindupindu kwa zaidi ya asilimia 90 ifikapo 2030. Hivyo, kikao hiki kina umuhimu mkubwa katika kubaini maeneo yaliyo hatarini na kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti,” alisisitiza. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Masuala ya Dharura kutoka Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika (WHO-AFRO), Dkt. Dick Chamla, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na WHO katika kupambana na magonjwa ya mlipuko, ikiwemo Kipindupindu. 

“Serikali ya Tanzania imeonyesha mfano wa kuigwa kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano haya. Kupitia kikao hiki, tunaamini tutaweza kuainisha maeneo hatarishi na kuchukua hatua sahihi kwa pamoja,” alisema Dkt. Chamla. 

Kwa mujibu wa WHO, Kipindupindu bado ni tishio kwa maisha ya watu wengi barani Afrika, hivyo ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau wa afya unahitajika ili kudhibiti mlipuko huo kwa ufanisi.



Chapisha Maoni

0 Maoni