Kamishna wa Uhifadhi
wa Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Bw. Abdul-razaq Badru
amewapongeza watumishi wa Mamlaka hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na kuiwezesha
Mamlaka hiyo kufikia malengo iliyojiwekea katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza katika
kikao kazi na watumishi wa NCAA tarehe 9 Juni, 2025 Karatu Mkoani Arusha
Kamishna Badru alieleza kuwa katika Mwaka wa fedha 2024/2025 Mamlaka hiyo
ilijiwekea lengo la kukusanya mapato ya shilingi Bilioni 230 lakini ikavuka
lengo hilo na kukusanya shilingi Bilioni 269.9 ambapo mapato yaliyokusanywa
kutokana na shughuli za utalii ni Bilioni 262.74, mapato ya Pori la akiba
Pololeti shilingi Bilioni 3.7 na mapato yaliyokusanywa kwenye vyanzo vingine
vya mamlaka hiyo ni Shilingi Bilioni 3.274.
Aidha, wageni
wanaotembelea hifadhi ya Ngorongoro wameongezeka kutoka wageni 908,000 mwaka
2023/2024 hadi kufikia wageni 1,061,620 mwaka wa fedha 2024/2025.
Badru amewashukuru
pia watumishi hao kuhamasisha upigiaji kura wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro
katika kinyang’anyiro cha World travel awards na kuiwezesha hifadhi hiyo
kutangazwa kuwa kivutio bora cha utalii Afrika mwaka (Africa’s leading tourist
attractions 2025) katika tuzo zilizotolewa tarehe 28 Juni, 2025.
Amebainisha kwa kuwa
sasa Mamlaka hiyo inaandaa mkakati wa miaka mitano ijayo ambapo mkakati
utashirikisha kila mtumishi kujiwekea shabaha, malengo yanayopimika katika
utendaji kazi na kubainisha kuwa mkakati huo utaendana na dira kuu ya taifa ya
mwaka 2050 ambayo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Mkakati wa NCAA
utajikita katika kusimamia uhifadhi endelevu, kutangaza vivutio vya utalii na
kuboresha miundombinu yote ya utalii ambayo inaenda sambamba na kuibua na
kuendeleza mazao mapya ya utalii na pia mkakati utajikita katika shughuli za
maendeleo ya jamii kwa wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo.
Kamishna Badru
amewasisitiza watumishi hao kuwa, ili kufikia malengo makubwa zaidi watumishi
wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, ufanisi, kutoa huduma bora na za viwango vya
kimataifa kwa wageni, kuzingatia sheria na maadili ambapo vikifanyika kwa
pamoja na kuweka mshkamano kwa watumishi wote itaiwezesha taasisi hiyo kutoa
huduma katika viwango vya kimataifa na kuendana na maono ya
viongozi wa Nchi.
Na. Mwandishi wetu -
Karatu Arusha
0 Maoni