Kelsey Bone na Scot
Pominville watalii kutoka Jimbo la Regina - Saskatchewan nchini Canada wamechagua
kufunga ndoa yao katika kileleni cha Uhuru kilichopo juu ya Mlima Kilimanjaro
badala ya kufanyia kwenye ukumbi wa harusi wa kawaida.
Ndoa hiyo imeifanyika
mapema mwezi Julai 2025, baada ya kupanda kwa siku sita hadi urefu wa futi
19,300, ambapo walibadilishana viapo vya ndoa wakiwa na marafiki zao wa karibu
na waongoza watalii watano (5).
Sherehe yao ya harusi
ilikuwa ya kipekee na ya kihisia, Bone alieleza kuwa licha ya upungufu wa
oksijeni, walihisi furaha ya kipekee kutokana na nyimbo na ngoma za waongoza
watalii waliokuwa pamoja nao. “Tukio letu likikuwa maalum sana kundi letu la
waongoza watalii waliokuwa wakiimba na kucheza kwa ajili yetu walikuwa
wanatufurahisha sana na kutufanya tujisikie vizuri muda wote,” alieleza Bone.
Licha ya baridi kali,
Bone alivaa gauni jeupe la harusi (Shera), alilolivaa chini ya suruali ya mvua,
huku Pominville akivaa koti lake la suti. Walihakikisha wanaheshimu tukio hilo
kwa mavazi rasmi, ijapokuwa mazingira hayakuwa rafiki.
Pominville alieleza kuwa
safari ya kuelekea kileleni haikuwa rahisi wala ya kifahari kama watu wengi
wanavyofikiria. “Sio tukio la kifahari sana hatukuweza hata kuoga kwa wiki
nzima,” Pominville alisema kwa kicheko.
Wawili hao walichumbiana
mwaka uliopita 2024 katika Kambi ya watalii iliyopo Mlima Everest, baada ya
kupanda kwa siku 10. Pominville alificha pete kwenye mfuko wa plastiki ili
isiweze kugundulika kabla ya kumvalisha Bone kwa mshangao mkubwa.
Mlima Kilimanjaro
umeendelea kuwa kivutio kikubwa barani Afrika kutokana na umaarufu wake wa kuwa
na kilele cha Uhuru ambacho ndicho kilele kirefu zaidi Afrika ukijulikana kama
Paa la Afrika. Pia ni Mlima uliosimama peke yake duniani huku ukiwa na uwanda
wa hali ya hewa tofauti tofauti pamoja na ukanda wa barafu hivyo, kuvutia
maelfu ya watalii kutoka kila kona ya ulimwengu.
0 Maoni