Ikiwa katika muendelezo
wa ziara yake ya kutembelea utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya
barabara, Kamati ya Ukaguzi ya TARURA
imetembelea Miradi minne ya ujenzi wa miundombinu ya barabara mkoani
Shinyanga.
Katika Manispaa ya
Shinyanga Kamati ilitembelea ujenzi wa barabara ya Old Shinyanga-Chibe-Negezi
kiwango cha changarawe na ujenzi wa
Kalavati na daraja la Mawe la Nin'ghwa katika barabara hiyo.
Vile vile kamati hiyo
ilipata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Kinyata-Karena yenye
urefu wa Km 0.8 kwa kiwango cha lami inayojengwa Kata ya Kambarage katika
Manispaa hiyo.
Pia, Kamati imetembelea
Mradi wa uondoaji vikwazo wa ujenzi wa Daraja la seli sita linalojengwa katika
barabara ya Magonzo-Shinyanga unaotekelezwa chini Mradi wa RISE pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara ya
DED-DC Km 1.0 kwa kiwango cha lami Wilayani Kishapu.
Akielezea manufaa ya
Miradi hiyo kiuchumi na kijamii, Meneja wa TARURA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi
Avith Rugemalila ameieleza Kamati hiyo kuwa itarahisisha huduma ya usafiri na
usafirishaji wa mazao na bidhaa ndani na nje ya Manispaa ya Shinyanga pamoja na
Wilaya ya kishapu.
"Miradi hii pia
itavutia biashara na uwekezaji katika Mkoa wetu na hatimaye kuongeza pato kwa
mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla," ameongeza Mhandisi Rugemalila.
Naye, Paulo Izengo Mkazi
wa Wilaya ya Kishapu ambaye ni bodaboda ameishukuru Serikali kwa kuwajengea
barabara hiyo kwani mazingira ya biashara yao yamekuwa mazuri na sasa gharama
za matengenezo ya bodaboda zimepungua na faida imeongezeka.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi TARURA CPA. Ally Rashid amesema kuwa lengo la
ziara hiyo ni kutembelea Miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, kusikia
changamoto kutoka TARURA Mkoa wa Shinyanga pamoja na Wakandarasi.
"Tunazichukua
changamoto zote na kuona namna gani tutashauri na pale ambapo mmefanya vizuri
vile vile ni kitu cha kupongeza ingawa sio kitu cha kupongeza sana kwa sababu
ni wajibu wenu vitu viende vizuri na ni sehemu ya uwajibikaji," amefafanua CPA. Rashid.
0 Maoni