Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametangaza kuwa CCM imeamua kufanya marekebisho ya Katiba yake ili kuruhusu Kamati Kuu ya chama hicho kuteua wagombea wengine zaidi ya majina matatu yaliyopitishwa na Kamati za Siasa za Wilaya na Mkoa, pale ambapo kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.

Akizungumza leo katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika jijini Dodoma, Dkt. Samia alisema mabadiliko hayo yanakusudia kuongeza ufanisi na kutoa nafasi kwa Kamati Kuu kuwa na mamlaka mapana zaidi ya uteuzi, hasa ikizingatiwa idadi kubwa ya wanachama wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali.

“Tulitanua demokrasia, wajumbe wa kuchagua wawe wengi zaidi. Jambo lile limevutia wanachama wengi wa CCM kuomba kugombea, na kuna maeneo yenye wagombea hadi 40. Tumeona kwenda na watatu kati ya wengi hao si busara, halafu papohapo Kamati Kuu imebanwa na Katiba, hatuwezi kuongeza majina,” alisema Rais Dkt. Samia.

Aliendelea kufafanua kuwa uamuzi huo ni sehemu ya mageuzi ndani ya chama yanayolenga kuendana na hali halisi ya kisiasa nchini. “Tumerudi kwenu kuomba ridhaa ya hilo, na sasa tunataka jambo hili lijadiliwe. Mjadala upo wazi,” aliongeza.

Kwa sasa, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wanaendelea na zoezi la kupiga kura ya ama kuidhinisha au kukataa pendekezo hilo la marekebisho ya Katiba.

Mabadiliko haya, iwapo yatapitishwa, yanatarajiwa kuongeza ushawishi wa Kamati Kuu katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM kuelekea uchaguzi mkuu ujao.