TFS yatangaza fursa za uwekezaji kwa vijana katika maonesho ya Iringa

 

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetumia jukwaa la Maonesho ya Ujuzi, Fani na Ajira kwa Vijana yanayoendelea katika viwanja vya Mwembe Togwa, Manispaa ya Iringa, kutangaza fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana kupitia uhifadhi wa misitu nchini.

Maonesho hayo yaliyoanza Julai 25 hadi 27, 2025, yanalenga kuhamasisha vijana wa Mkoa wa Iringa na maeneo jirani kujikita katika sekta zinazoweza kuwainua kiuchumi, zikiwemo ufugaji nyuki, biashara ya mazao ya misitu, upandaji miti, pamoja na utalii wa ikolojia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Mhe. Estomih Kyando, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa, aliipongeza TFS kwa kuendelea kutoa elimu na kufungua milango ya fursa kwa vijana kupitia ushiriki wao katika maonesho hayo.

“Mkoa wetu wa Iringa una historia nzuri ya uhifadhi wa misitu na wananchi wake wameonyesha mwitikio mkubwa katika biashara ya mazao ya misitu ya kupandwa. TFS imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi za fursa hizi,” alisema Mhe. Kyando.

Alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa mabalozi wa elimu ya uhifadhi na wawe mstari wa mbele kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta mbalimbali zinazochochewa na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya maendeleo jumuishi kwa vijana kupitia ujuzi, ajira na uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake, Mhifadhi Paulo Rugola kutoka TFS, akizungumza wakati wa ziara ya viongozi wa serikali katika banda lao Julai 26, 2025, alieleza kuwa TFS inatumia majukwaa ya maonesho kama haya kuwafikia wananchi na kuwahamasisha kuhusu matumizi endelevu ya misitu kwa ajili ya maendeleo yao ya kiuchumi.

“Tunatangaza fursa mbalimbali zilizopo katika misitu yetu. Hizi ni pamoja na upatikanaji wa malighafi kutokana na miti, ufugaji nyuki na uuzaji wa mazao yake, pamoja na utalii wa ikolojia ambao unaendelea kukua kwa kasi nchini,” alisema Rugola.

Aliongeza kuwa TFS ina vituo maalum vya uzalishaji wa mbegu bora za miti kwa ajili ya wananchi wanaotaka kuwekeza kwenye kilimo cha miti, hasa katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini ambapo uelewa kuhusu faida ya misitu umeongezeka.

“Tunawakaribisha vijana na wakulima wote kuja kujifunza kuhusu uzalishaji bora wa miti, kwani upandaji miti siyo tu unaongeza kipato, bali pia ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisisitiza Rugola.

Aidha, alikemea matumizi holela ya moto katika maeneo ya misitu hasa msimu huu wa kiangazi, akihimiza wananchi kuchukua tahadhari na kufuata elimu ya uhifadhi wanayopewa na maafisa wa TFS.

“Kumekuwa na matukio mengi ya moto ambayo yanaharibu juhudi kubwa za kuhifadhi misitu. TFS inaendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya moto ili kulinda rasilimali hizi kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” aliongeza.

TFS ni miongoni mwa taasisi nyingi za serikali na binafsi zinazoshiriki katika maonesho hayo yaliyoandaliwa kwa kauli mbiu: “Kijana: Ujuzi Wako, Fani Yako, Chaguo Lako.” Maonesho haya yanatarajiwa kufungwa rasmi Julai 27, 2025.




Chapisha Maoni

0 Maoni