Eneo la hifadhi ya
Ngorongoro limeendelea kuwa kimbilio la wageni mashuhuri duniani ambapo siku ya
leo, Meya wa Jiji la Dallas nchini
Marekani, Mhe. Eric Johnson kwa mara ya kwanza ameshuhudia upekee wa vivutio
vya utalii vilivyopo katika hifadhi hiyo.
Meya huyo
aliyefuatana na Balozi wa Tanzania
nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza amepokelewa na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Eneo la Ngorongoro (NCAA), Abdul-Razaq Badru na kuwaeleza kuwa eneo la hifadhi
ya Ngorongoro lina utajiri wa vivutio vya utalii ikiwepo Kreta ya Ngorongoro,
Wanyama wakubwa watano "Big Five",
bonde la Olduvai lenye gunduzi mbalimbali za Zamadam, tambarare za Ndutu
ambazo ni mazalia ya Nyumbu, mchanga unaohama, Nyayo za Laetoli zenye umri wa
miaka Mil 3.7 iliyopita na vivutio vingine vingi.
Kamishna Badru alieleza kuwa Ngorongoro si tu
kivutio cha utalii bali ni ni somo la
uhai linaloishi.
“Hapa ndipo unaweza
kuwaona faru weusi katika mazingira yao ya asili, jambo ambalo ni nadra
duniani. Na juhudi zetu za kulinda viumbe hawa walio hatarini kutoweka
zinaendelea ili kuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo,” alisisitiza.
Kwa upande wa Kamishna
Msaidizi Mwandamizi, Huduma za Utalii na Masoko, Mariam Kobelo, alieleza kuwa
hifadhi ya Ngorongoro ni eneo lenye hadhi tatu za kimataifa zinazotambuliwa na UNESCO ambazo ni
Hifadhi ya Binadamu na Baiolojia, Urithi wa Dunia Mchanganyiko unaojumuisha
maliasili na utajiri wa kiutamaduni unaoshikilia historia ya mwanadamu na hadhi
ya tatu ni eneo lenye hadhi ya utalii wa miamba (Ngorongoro Lengai Global
Geopark).
Akielezea furaha yake
baada ya kufika hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni kivutio namba moja cha utalii
Afrika Meya Eric Johnson amesema kuwa; “Huu ni uzuri usioelezeka, ni mara yangu
ya kwanza kufika Afrika, na hapa Ngorongoro nimeshuhudia wanyama wa kila aina,
mandhari ya kuvutia, na mfumo wa ikolojia ambao ni wa kipekee duniani. Naahidi
kurudi tena na familia yangu.”
0 Maoni