Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amekabidhi Leseni ya Utafiti na Uchimbaji Mkubwa wa Madini Adimu na Muhimu ambayo ni ya kimkakati ya Rare Earth Elements (REE) kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ikiwa ni hatua muhimu ya kuliwezesha shirika kuingia kwenye shughuli za uchimbaji mkubwa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wote wa Tanzania.
Makabidhiano hayo
yamefanyika leo Julai 24, 2025 katika viwanja vya Shule ya Msingi Sesenga
kijiji cha Sesenga Kata ya Mgazi Wilaya ya Morogoro, kufuatia uamuzi wa
Serikali wa kuirejesha leseni hiyo kutoka kwa kampuni ya Wigu Hill Mining
Company Limited baada ya kumalizika kwa shauri la madai kwenye Baraza la
Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji(ICSID).
Akizungumza mbele ya
mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye hafla ya makabidhiano
ya leseni hiyo, Waziri Mavunde amesema kuwa madini ya Rare Earth Elements ni
miongoni mwa madini ya kimkakati ambayo kwa sasa yanahitajika kwa kiwango
kikubwa duniani kutokana na umuhimu wake
katika sekta ya teknolojia ya kisasa.
"Madini haya
yanatumika katika vifaa vya kivita, kutengeneza simu janja, kompyuta, betri za
magari ya umeme, vifaa vya matibabu na mashine mbalimbali. Hii ni fursa adhimu
kwa kijiji cha Sesenga, Wilaya ya Morogoro, Mkoa na Taifa kwa ujumla kunufaika
na rasilimali hii muhimu," amesisitiza Waziri Mavunde.
Pia, Waziri Mavunde
amebainisha kuwa mradi huo utafungua fursa nyingi za ajira kwa wakazi wa maeneo
ya jirani na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kupewa kipaumbele
kwa wananchi wanaozunguka mgodi kuuza bidhaa zao mgodini (Local content) na kupitia
uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).
Vilevile, ameeleza kuwa
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro itaongeza mapato yake kupita tozo za huduma
ambazo hutozwa kwenye shughuli za madini.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mavunde ameitaka STAMICO kuanza mara moja mchakato wa uendelezaji wa
leseni hiyo ili shughuli za uzalishaji madini hayo ziweze kuanza kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala amempongeza Waziri Mavunde kwa kuisimamia
vizuri Sekta ya Madini na kumuahidi Waziri huyo kuendelea kusimamia sekta hiyo
kwa karibu kwa ajili ya masilahi ya taifa.
Naye, Katibu Mkuu Wizara
ya Madini Eng. Yahya Samamba amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa
kuweka mazingira rafiki na salama kwenye maeneo ya uchimbaji madini nchini ambapo
kwa sasa wachimbaji wananufaika na rasilimali hiyo.
Aidha, Mkurugenzi
Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, ameishukuru Serikali kupitia Wizara
ya Madini kwa kuendelea kuwaamini na kulikabidhi shirika hilo leseni hiyo
muhimu na kumhakikishia Waziri Mavunde kuwa STAMICO iko tayari kuanza kazi kwa
wakati na kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi, kwa muda
uliopangwa na kwa kuzingatia manufaa mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
"Tunatambua wajibu
wetu mkubwa kwa taifa, STAMICO iko tayari kusimamia mradi huu kwa weledi wa
hali ya juu ili kuleta tija na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika Pato
la Taifa," amesema Dkt. Mwasse.
Uamuzi wa Serikali
kukabidhi leseni hiyo kwa STAMICO ni sehemu ya jitihada za kulinda maslahi ya
Taifa katika Sekta ya Madini kwa kuhakikisha maeneo yenye rasilimali hayakai
bila kuendelezwa na kwamba rasilimali hizo zinachangia moja kwa moja katika
ustawi wa wananchi na uchumi wa nchi.
0 Maoni