Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa vyombo vya habari kushirikiana na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu historia ya mashujaa nchini.
Dkt. Biteko ametoa wito
huo Julai 24, 2025 katika Uwanja na Mnara wa Mashujaa uliopo Mji wa Serikali,
Mtumba jijini Dodoma mara baada ya kukagua maadalizi ya Maadhimisho ya Siku ya
Mashujaa.
“ Ninatoa wito kwa
wananchi wote kushiriki kwa wingi kwenye tukio hili adhimu. Hii ni siku yetu
sote, siku ya kumkumbuka Mtanzania mwenzetu aliyesimama kwa ajili ya Taifa.
Vivyo hivyo, nawaomba nyinyi waandishi wa habari, pamoja na vyombo vyenu na pia
mitandao ya kijamii mshirikiane na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu
historia ya mashujaa wetu, thamani ya mchango wao, na sababu ya sisi kuendelea
kuwakumbuka kila mwaka,” amesema Dkt. Biteko.
Amezungumzia maandalizi
ya Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa na kusema kuwa yanaendelea vizuri na mgeni
rasmi katika tukio hilo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akisisitiza kuwa siku hiyo ni
maalum kwa ajili ya kuwakumbuka, kuwaenzi na kuwaheshimu mashujaa wetu waliotoa
maisha yao, nguvu zao, na sadaka zao kwa ajili ya uhuru, amani na maendeleo ya
Taifa.
Amefafanua kuwa kwa
heshima hiyo, saa 6:00 usiku wa tarehe 24 Julai, 2025 siku moja kabla ya kilele
cha maadhimisho, Mwenge wa Kumbukumbu ya Mashujaa utawashwa rasmi na Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule kwa niaba ya Rais kuashiria kuanza kwa
maombolezo ya Mashujaa wetu.
Ameongeza kuwa katika
siku ya maadhimisho kesho tarehe 25 Julai, 2025 kuanzia saa 3:00 asubuhi
kutakuwa na gwaride rasmi la heshima litakalofanywa na Vikosi vya Ulinzi na
Usalama. Aidha, saa 6:00 usiku wa tarehe hiyohiyo mwenge wa Kumbukumbu ya
Mashujaa utazimwa rasmi kuashiria hitimisho la maombolezo ya kumbukumbu
Mashujaa kwa mwaka 2025.
Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa hufanyika kila mwaka tarehe 25 Julai 2025 kwa lengo la kuwakumbuka mashujaa waliopoteza maisha yao katika uwanja wa vita, waliostaafu baada ya kulitumikia Taifa kwa uaminifu, na wale waliopata majeraha katika kuilinda nchi yetu.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni