Imeelezwa kuwa kukamilika
kwa daraja la Masagi linalojengwa katika barabara ya Kibirigi-Masagi kutasaidia
kuunganisha vijiji vya Kibirigi, Masagi na Tyeme katika Kata ya Mtoa, Wilaya ya
Iramba mkoani Singida.
Hayo yameelezwa na Meneja
wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Ibrahim Kibasa wakati akitoa taarifa ya
utekelezaji wa Mradi huo mbele ya Kamati ya Ukaguzi ya TARURA inayofanya ziara
ya Ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa Miundombinu ya barabara mkoani humo.
"Vijiji vya
Kibirigi, Masagi na Tyeme vinajishughulisha na shughuli za kilimo hususani
pamba, alizeti, dengu, mahindi pamoja na ufugaji, hivyo kukosekana kwa daraja
katika Mto sekenke linapojengwa daraja hilo ilikuwa ni kikwazo kwao katika
kuyafikia masoko ya mazao yao na kurudisha nyuma jitihada za kujiletea
maendeleo," amefafanua Mhandisi Kibasa.
Kwa mujibu wa Mhandisi
Kibasa kukamilika kwa Mradi huo utachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii
katika vijiji hivyo na kuchangia ustawi wa maendeleo ya Wilaya na Taifa kwa
ujumla.
Mhandisi Kibasa ameileza
Kamati hiyo kuwa licha ya changamoto ya mvua iliyojitokeza katika hatua ya
utekelezaji, mradi huo umefikia hatua ya kuridhisha na matarajio yake ni kuwa
utakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TARURA CPA Ally Rashid amemtaka Meneja wa
TARURA Mkoa wa Singida na timu yake kuendelea kumsimamia Mkandarasi
anayetekeleza Mradi huo kuzingatia ubora sambamba na kuyafanyia kazi mapungufu
kadhaa waliyoyabaini wakati wa Ukaguzi wao katika Mradi huo.
0 Maoni