Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ametumia ziara yake nchini
Belarus kunadi fursa za uwekezaji katika maeneo manne ya kipaumbele ya Serikali
ya awamu ya sita ambayo ni kilimo, afya, madini na ulinzi & usalama.
Mhe. Waziri Mkuu katika
siku mbili za ziara yake, tarehe 22 na
23 Julai 2025 ametembelea kampuni kubwa nane zenye nguvu ya mitaji jijini Minsk
na kuzihakikishia utayari wa Serikali ya Tanzania kushirikiana nazo kwa
kuzipatia kila aina ya msaada zitakapokuja Tanzania kuwekeza.
Kwenye eneo la kilimo,
Mhe. Waziri Mkuu alikutana na viongozi wa kampuni ya AFTRADE ambayo tayari ipo
nchini na kuwasisitiza kuongeza kasi katika kuendeleza kilimo hususan kuwa na
programu za kuwasaidia wakulima wadogo mitaji, utafiti na mafunzo ili
kilimo kiweze kuwa na tija, kizalishe
ajira na kuongeza usalama wa chakula nchini.
Katika eneo hilo la
kilimo, Waziri mkuu pia alitembelea chuo cha kilimo cha Belarus na viwanda vya
matrekta na kuvishawishi viwanda hivyo
kufungua matawi nchini Tanzania.
Kuhusu chuo cha kilimo
ambacho mafunzo yake huyafanya kwa vitendo zaidi, Waziri Mkuu aliomba Watanzania wapatiwe fursa
za masomo katika chuo hicho ili waweze kuendeleza sekta ya kilimo nchini,
watakapomaliza masomo yao.
Kuhusu Afya, Mhe. Waziri
Mkuu alitembelea kampuni ya kuzalisha na kusambaza dawa na vifaa tiba ya
Belmedepreparaty ambayo ni moja ya kampuni kubwa nchini Belarus. Kampuni hiyo
inayozalisha bidhaa tofauti tofauti zaidi ya 1700 na kuuza ndani na nje ya nchi
katika mataifa zaidi ya 24, iliridhia maombi ya Mhe. Waziri Mkuu na kuahidi
kufanya ziara nchini Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji.
Mhe. Waziri Mkuu alisema
Belmedepreparaty ni kampuni sahihi kuja kuwekeza nchini kutokana na kutumia
teknolojia ya kisasa ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa.
Kwa upande wa sekta ya
madini, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kutengeneza mitambo inayotumika
kuchimba madini migodini na kukishawishi kiwanda hicho kuja kuwekeza nchini
Tanzania.
Kuhusu suala la Ulinzi na
Usalama, Mhe. Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kutengeneza vifaa vya ukoaji
na kuzima moto na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana na kiwanda hicho ili
kuondoa tatizo la uhaba wa vifaa hivyo nchini.
Waziri Mkuu amemaliza
ziara yake na aliondoka Julai 24, 2025 kurejea nyumbani.
0 Maoni