Ujumbe wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ukiongozwa na Mwakilishi Mkazi, Shigeki
Komatsubara, kwa kushirikiana na ujumbe wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
(TFS) ukiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, umetembelea
Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia wa Ziwa Duluti jana Julai 23, 2025.
Ziara hiyo imelenga
kujionea maendeleo ya maboresho katika uhifadhi na miundombinu ya utalii,
ambayo inalenga kuvutia wageni zaidi katika hifadhi za misitu ya asili nchini.
UNDP ni mshirika mkuu wa
utekelezaji wa mradi wa kitaifa unaoitwa “Kujenga Ustahimilivu wa Bioanuwai ya
Misitu Dhidi ya Matishio ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Hifadhi za
Misitu ya Mazingira Asilia Tanzania”.
Mradi huo wa miaka sita,
wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 15, unafadhiliwa na Mfuko wa
Mazingira Duniani (GEF) kupitia UNDP na unatekelezwa kwa kushirikiana na TFS
katika hifadhi mbalimbali za misitu ya mazingira asilia.
Umezinduliwa rasmi mapema
mwaka huu na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, katika
Msitu wa Pugu-Kazimzumbwi, mkoani Pwani.
Lengo kuu la mradi huo ni
kuimarisha ustahimilivu wa bioanuwai ya misitu dhidi ya athari za mabadiliko ya
tabianchi, huku ukichangia maendeleo endelevu ya jamii zinazozunguka hifadhi
hizo.
Ziara ya Duluti imefuatia
Mkutano wa Tatu wa Kamati ya Uendeshaji wa Mradi, uliofanyika Julai 22, 2025
katika Ukumbi wa Ngorongoro, Arusha, ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, aliongoza kama
Mwenyekiti wa kikao hicho.
0 Maoni