Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula,
amemkabidhi rasmi Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Press Card) kwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Michuzi Media Group, Bw. Muhidin Issa Michuzi, kwa niaba
ya waandishi wa habari wengine waliokidhi vigezo vya kisheria vya kupatiwa
vitambulisho hivyo.
Makabidhiano hayo
yamefanyika katika ofisi za JAB jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa jukumu la bodi hiyo kuhakikisha waandishi wote nchini wanatambulika
kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016.
Akizungumza baada ya
kukabidhi kitambulisho hicho, Wakili Kipangula amempongeza Bw. Michuzi na
waandishi wengine waliokwishakamilisha taratibu za kupata vitambulisho vyao,
akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa ustawi na weledi wa tasnia ya habari
nchini.
Ameeleza kuwa bado kuna
waandishi wengi ambao maombi yao yamesalia katika hatua ya uhakiki kutokana na
changamoto mbalimbali, hususan mapungufu katika viambatisho walivyowasilisha
kwenye mfumo wa maombi.
“Mfumo wetu unakagua
nyaraka zote kwa uangalifu. Tumebaini maombi mengi yameambatanishwa na nyaraka
zisizosoma, nyingine zimejirudia, nyingine zina viambatisho visivyotambulika
kisheria kama vile vyeti bandia, na baadhi hawajaambatanisha hata barua za
utambulisho kutoka kwa waajiri wao,” alisema Kipangula.
Aidha, amewataka
waandishi wa habari ambao bado hawajapata vitambulisho vyao kuhakikisha
wanaingia tena kwenye akaunti zao za mtandaoni kupitia mfumo wa JAB, na
kuhakiki nyaraka walizoweka, kama zinafunguka na kusomeka ipasavyo kabla ya
kupiga simu kuhoji hali ya maombi yao.
Kwa mujibu wa Kipangula,
Bodi itaendelea kupitia maombi kwa makundi kadri yanavyowasilishwa, huku
ikiweka msisitizo kwa waandishi kuhakikisha wanatimiza vigezo vyote
vilivyoainishwa katika mwongozo wa kisheria uliotolewa.
Makabidhiano hayo
yanakuja wakati ambapo serikali imeendelea kuhimiza weledi, uwajibikaji, na
utii wa sheria miongoni mwa wanahabari nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za
kulinda uhuru wa vyombo vya habari sambamba na kuhakikisha maadili ya taaluma
hiyo yanazingatiwa.
0 Maoni