Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuwa Hayati Mzee Mkapa atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi cha sasa na kijacho kutokana na mchango wake mkubwa katika kujenga misingi ya maendeleo, utawala bora na ustawi wa Taifa. Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijenga nguzo muhimu za umoja wa kitaifa, Muungano, amani na mshikamano wa Watanzania, pamoja na nafasi ya Tanzania katika bara la Afrika na ulimwenguni.
Rais Dkt. Mwinyi
ameyasema hayo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ibada Maalum ya Kumbukumbu ya Miaka Mitano ya
Hayati Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, iliyofanyika leo tarehe 23 Julai 2025 Lupaso, Wilaya ya
Masasi, Mkoa wa Mtwara.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi
amekumbusha kuwa Hayati Mzee Mkapa alikuwa muumini wa ujamaa na uchumi wa soko
unaoongozwa na sekta binafsi, lakini pia alihakikisha kuwa maendeleo
yanawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi. Ameeleza kuwa Hayati Mzee Mkapa
ndiye aliyeanzisha Dira ya Maendeleo 2025, ambayo imekuwa chombo muhimu katika
mageuzi ya maendeleo, na mafanikio yake yamekuwa msingi wa kuzinduliwa kwa Dira
mpya ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Halikadhalika, Rais Dkt.
Mwinyi ametoa wito kwa viongozi wa dini, wanasiasa na wanahabari kuwa sehemu ya
kulinda na kuendeleza tunu ya amani kama njia ya kumuenzi Hayati Mkapa. Amesema
kuwa Watanzania wanayo sababu ya kujivunia viongozi waliopo ambao wanaendeleza
maono ya viongozi waasisi na kuipeleka Tanzania mbele katika nyanja zote za
maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi alizuru
kaburi la Hayati Benjamin William Mkapa na kuweka shada la maua, akiongozana na
Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi, na Mkewe pamoja na Mjane wa Hayati
Mkapa, Mama Anna Mkapa. Hayati Mzee Mkapa alifariki dunia usiku wa kuamkia
tarehe 24 Julai 2020 akiwa na umri wa miaka 81, jijini Dar es Salaam.
0 Maoni