Wizara ya Maliasili na
Utalii imepongezwa kwa kutekeleza kikamilifu maono ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa Wizara ya kwanza
kukamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi na kuwezesha Idara na Vitengo vyake
kuhamia Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Pongezi hizo zimetolewa
na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. William Lukuvi alipotembelea
Wizara hiyo kwa lengo la kukagua ujenzi wa Majengo ya Serikali ambao ni
utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Samia Suluhu ya Serikali kuhamia Dodoma.
Mhe. Lukuvi amesema kuwa
Wizara ya Maliasili na Utalii licha ya kukamilisha mapema ujenzi wa jengo hilo,
inastahili pia kupongezwa kuwa wa kwanza kuhamia na kuwa mfano katika Matumizi ya samani za Ofisini
zilizozalishwa hapa nchini kupitia mazao ya Misitu.
"Ninyi ni mabalozi
wazuri wa Matumizi ya bidhaa zetu za hapa nchini zinazotokana na Misitu yetu,
niimani yangu kuwa Wizara zote zitaiga mfano huu," aliongeza Mhe. Lukuvi.
Aidha Mhe. Lukuvi ametoa
rai kwa watumishi wa Wizara hiyo kuhakikisha wanatunza vyema miundombinu na
vifaa vilivyopo ili viweze kudumu kama ilivyo kusudiwa.
Naye Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amemshukuru Waziri Lukuvi kwa
ziara yake, na kuahidi kuwa Wizara itatekeleza vyema maelekezo aliyoyatoa
hususani ya usimamizi mzuri wa Matumizi ya jengo na vifaa vilivyopo.
0 Maoni