Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi ya donge nono ya fedha taslimu Shilingi Bilioni 1 iwapo timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars watafanikiwa kutwaa Ubingwa wa CHAN 2024 ambayo yanafanyika mwaka huu kwa pamoja katika mataifa matatu ya Tanzania, Kenya na Uganda.
Akizungumza na Waandishi
wa habari Jijini Dar es Salaam Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Mhe. Palamagamba Aidan Mwaluko Kabudi amesema Rais Samia ametoa ahadi ya kitita
cha fesha Shilingi Billioni 1 endapo timu hiyo itatwaa ubingwa huo wa CHAN
2024.
"Katika kuchagiza
hamasa kwa timu yetu ya Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi ya donge nono Shilingi Bilioni 1 kwa
vijana wetu wa Taifa Stars wakifanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano haya ya
CHAN 2024," amesema Waziri Kabudi.
Aidha, Waziri Kabudi
amesema Tanzania haijapata nafasi hiyo kwa bahati mbaya ni kutokana na
uwekezaji na hamasa ya Rais Samia katika uwekezaji kwenye sekta ya michezo.
Katika upande mwingine
waziri Kabudi amesema maandalizi mengine muhimu ya mashindano hayo
yameshafanyika ikiwemo maandalizi ya mchezo wa ufunguzi, kufanya malipo ya
gharama za ada, maandalizi ya viwanja vya mashindano pamoja na mazoezi.
Kisha Waziri akatoa wito
kwa watanzania kuchangamkia fursa za kibiashara na uchumi ikiwemo vyakula
malazi na usafirishaji kwa wakati huu wa mashindano ya CHAN.
Kwa upande wa hamasa
Waziri amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi katika kuishangilia timu ya
Taifa kama kaulimbiu iliyozinduliwa katika Uwanja wa Zakhiem Mbagala ya LINAKUJA NYUMBANI.
Pia kutakuwepo na hamasa
kubwa kwa siku mbili kabla ya mashindano ambapo kutafanyika tamasha la muziki
wa Singeli litalalojulikana kama CHAN SINGELI FESTIVAL kwa lengo pia la
kuhamasisha muziki huo kimataifa.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Gerson Msigwa amesema kutakuwepo na zawadi ya goli la mama
ambapo itatoka zawadi ya Milioni 10 kwa kila goli watakalofunga Taifa Stars
katika michezo ya makundi na mtoano na zawadi
itapanda hadi shilingi millioni 20 kwa kila goli watalalofunga kwenye
mechi za nusu fainali na fainali.
Mchezo wa ufunguzi wa
mashindano hayo utafanyika Agosti 2 katika Uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar
es Salaam ambapo timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars itashuka dimbani
kucheza na Burkina Faso na mgeni rasmi wa mchezo huo anatarajia kuwa Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.
0 Maoni