Serikali kupitia Wakala
wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza rasmi ujenzi wa daraja jipya la kisasa
katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa
muda mrefu wa kutatua tatizo sugu la mafuriko linalolikumba jiji hilo hasa
nyakati za mvua kubwa.
Daraja hilo, litakalokuwa
na urefu wa mita 390, linajengwa kwa viwango vya juu vya kisasa likilenga
kuhakikisha uimara, usalama na matumizi ya muda mrefu, hasa kwa kuzingatia
athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuathiri maeneo mengi ya
mijini.
Meneja wa TANROADS Mkoa
wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, ameeleza kuwa tayari mkandarasi
wa mradi amepokea malipo ya awali na kazi ya awali ya kutengeneza barabara ya
muda (diversion) kwa ajili ya magari imeanza.
“Daraja hili ni la
kimkakati kwa kuwa linashughulikia tatizo la muda mrefu la mafuriko eneo la
Jangwani. Pia litasaidia kuboresha usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam, kwa
kuwa litajumuisha pia njia za magari, maingilio pamoja na njia salama za waenda
kwa miguu,” alisema Mhandisi Kyamba.
Ameeleza kuwa mradi huo
ni sehemu ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan, katika kuboresha miundombinu ya jiji la Dar es Salaam na kulifanya kuwa
na uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Jangwani ni miongoni mwa
maeneo yanayokumbwa mara kwa mara na mafuriko wakati wa mvua, hali
inayosababisha usumbufu kwa wakazi, hasara kwa wafanyabiashara pamoja na
kuathiri shughuli za usafirishaji. Ujenzi wa daraja hili unatarajiwa kuwa
suluhisho la kudumu kwa tatizo hilo.
0 Maoni