Kamishna wa Uhifadhi,
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) CPA Musa Nassoro Kuji, amefanya ukaguzi katika eneo la vivuko vya
nyumbu (Kogatende) ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti. Katika ukaguzi huo
alielekeza Maafisa na Askari Uhifadhi kusimamia sheria ipasavyo, taratibu na
miongozo mbalimbali ya Hifadhi za Taifa ili kuboresha shughuli za utalii
endelevu usioharibu mazingira.
Ziara ya Kamishna Kuji aliyoifanya
jana ni muendelezo wa ziara zake za kikazi kukagua shughuli za maendeleo na
utekelezaji wa miongozo mbalimbali iliyowekwa na Wizara ya Maliasili na Utalii
ili kuwa na uhifadhi endelevu ambao ndio kiini cha utalii tunaoushuhudia leo
ukilipatia Shirika na Taifa mapato na fedha za kigeni ambazo zimeendelea
kuchagiza katika uchumi wa Taifa letu.
Akizungumza katika ziara
hiyo Kamishna Kuji alitoa maagizo kwa Maafisa na Askari Uhifadhi wanaosimamia
shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kuendelea kusimamia
sheria, kanuni na taratibu zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ili kuboresha huduma bora kwa watalii na kuwakumbusha kuzifuata ili kuondoa
mkanganyiko wa mara kwa kwa mara.
Aidha, Kamishna Kuji
alisema, “Endeleeni kuchukua tahadhari na kuendelea kusimamia taratibu na
sheria za hifadhi zilizowekwa kwa ajili ya kudhibiti vitengo vya uvunjifu wa
sheria na miongozo ya hifadhi iliyowekwa. Kuweni imara kudhibiti matendo
yanayokiuka taratibu zote za kiuhifadhi zinazofanywa na waongoza utalii wasio
na weledi kama vile kushusha watalii kwenye
magari maeneo yasiyoruhusiwa ambayo ni hatari kwa watalii na waongoza
watalii pia”.
Vilevile, CPA Kuji aliongeza,
Simamieni na kuthibiti magari yanayotumia njia zisizo halali na rasmi “Offroading”, kutupa taka hifadhini,
mwendokasi na tabia ya kulisha wanyamapori, kwa wale watakaokengeuka na kutotii
sheria na taratibu hizo, sheria ichukue mkondo wake”.
Naye, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Uhifadhi Stephano Msumi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa
Serengeti akitoa taarifa ya tukio lililotokea Julai 21, 2025 ambapo picha
jongefu na mnato zilionekana katika mitandao ya kijamii zikionesha watalii
wakiwa wameshuka kutoka kwenye magari katika eneo la Kogatende kivuko namba nne
wameshajulikana na taratibu za adhabu zinaendelea kuchukuliwa kwa kufuata
miongozo na hatutamuonea mtu wala kumfumbia mtu macho.
“Hata hivyo, Afande
Kamishna, kama hifadhi hii mama na yenye watalii wengi tumeshachukua hatua kali
za kisheria kutokana na tukio hilo ambapo kampuni zote zilizohusika kuvunja
sheria na taratibu kwa kushusha watalii kutoka kwenye magari yao katika maeneo
ambayo hayaruhusiwi tayari zimeanza kuchukuliwa,”alisema Mhifadhi Msumi.
Kamishna Msumi aliongeza
kuwa “Ni jukumu la kila mmoja wetu kwa maana ya TANAPA, waongoza watalii,
madereva pamoja na wadau wote wa utalii kuhakikisha kuwa tunafuata sheria,
taratibu na miongozo iliyowekwa tuwapo hifadhini ili kuendelea kutunza maliasili
zetu ambazo ni chanzo cha kuleta watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani. Na watalii hao hukuza uchumi wa watanzania
pamoja na kuchangia kuongeza pato la Taifa.
Katika kuhitimisha ziara
yake Kamishna Kuji ametoa maelekezo kwa uongozi wa Kanda ya Magharibi na
Hifadhi ya Taifa Serengeti kuongeza nguvu katika kuimarisha shughuli za ulinzi
na usalama katika eneo la Nyatwali Wilayani Bunda ambalo Shirika limekabidhiwa
kwa ajili ya kulijumuisha kuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa manufaa
ya shughuli za uhifadhi na utalii hapa nchini.
Na. Philipo Hassan -
Serengeti
0 Maoni