Kukamilika kwa ujenzi wa
daraja la zege katika Mto Kinkungu lenye urefu wa mita 65.6 linalojengwa katika
barabara ya Mtoa-Ndago Kata ya Shelui Wilayani Iramba kutanufaisha wananchi wa
Kata tano Wilayani humo.
Hayo yamebainika wakati
wa ziara ya Kamati ya Ukaguzi ya TARURA ikihitimisha Ukaguzi wa miradi ya
ujenzi wa miundombinu ya barabara mkoani Singida.
Meneja wa TARURA Mkoa wa
Singida Mhandisi Ibrahim Kibasa ameileza Kamati hiyo kuwa Mradi wa ujenzi wa
daraja hilo unalenga kuboresha mawasiliano kati ya Kata za Shelui, Mtoa, Ndago,
Mtekente na Urughu na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutachochea shughuli za
maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii katika Kata hizo.
"Licha ya changamoto
zilizojitokeza katika hatua za utekelezaji, mradi umefikia hatua ya kuridhisha
na matarajio ni kuwa utakamilika ndani ya muda uliopangwa ambao ni Septemba 15, 2025," alisema.
Akielezea hali ilivyokuwa
hapo awali Mzee Ali Hassan Jumanne ambaye ni Mkazi wa Shelui amesema kuwa hali
ilikuwa mbaya, watu walikuwa wanahatarisha maisha yao kuvuka mto Kinkungu hasa
kipindi cha masika ambapo maji hujaa katika Mto huo na wale waliokuwa
wakijaribu kuvuka walisombwa na maji.
"Tunaishukuru
Serikali kwa kutujengea daraja hili, tunamshukuru Rais Mama Samia kwani huko
nyuma tuliahidiwa kujengewa daraja hili na haikuwa hivyo lakini alipoingia
madarakani Mama Samia amefanya ndoto zetu kuwa za kweli, tunamshukuru sana
Mama".
Akitoa taarifa ya
majumuisho ya ziara yao ya Ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara katika
Mkoa wa Singida, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TARURA CPA. Ally Rashid
amesema kuwa kimsingi miradi yote waliyoitembelea kwa ujumla wake hatua
iliyofikia sio mbaya ni hatua nzuri isipokuwa inahitajika kuendelea na
usimamizi na kuhakikisha yale mapungufu machache ambayo wameyainisha
yanafanyiwa kazi katika hatua hiyo ya mwisho ya ukamilishaji wa miradi hiyo.
Katika taarifa hiyo pia
amesisitiza suala la uzingatiaji wa ubora katika utekelezaji wa miradi na sio
kukimbizana na muda tu hususani kwenye Miradi ya dharura sambamba na
utekelezaji wa miradi hiyo iendane na thamani ya fedha zilizotumika.
0 Maoni