Tasnia ya habari
nchini inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kabla na baada
ya uhuru ambapo uwepo wa baadhi ya vyombo vya habari vya awali kama vile gazeti
la Sauti ya TANU na redio Sauti ya Dar es Salaam vilisaidia kutoa mchango
mkubwa katika kujenga umoja, utaifa na kuhamasisha ushiriki wa harakati za
kudai uhuru.
Akizungumza Julai 9,
2025 jijini Dar es salaam wakati akifungua Mkutano wa Wadau Kujadili Mchango wa
Sekta ya Habari katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu 2025, Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa waandishi wa habari nchini
kuwa walinzi wa ukweli, wajenzi wa amani na wachochezi wa uwajibikaji wa
kisiasa.
Sambamba na
kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinabaki kuwa kioo safi cha jamii kisicho na
doa la uzushi, chuki au upendeleo na kuendelea kuhimiza maelewano, uvumilivu wa
kisiasa, na utamaduni wa kuheshimu tofauti za maoni.
“ Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa
waandishi wa habari katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi wanabaki
salama wao pamoja na mali zao. Aidha, Serikali, tutaendelea kulisimamia hili
kwa nguvu zetu zote. Tutahakikisha kuwa, mnakuwa na mazingira salama, huru na
rafiki wakati wote wa majukumu yenu, amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea kusema
katika kuelekea Uchaguzi Mkuu 20205 katika jamii kutakuwa na watu wenye mitazamo
mbalimbali kulingana na vipaumbele vyao hata hivyo vyombo vya habari vina fursa
ya kutoa uelekeo kwa taifa.
“Uchaguzi ni kipindi
cha muda mfupi, tumuombe Mungu hata
baada ya Uchaguzi tubaki kuwa Taifa moja lenye ustahimilivu na kila
mmoja akitoka kwake aende kutafuta mkate arudi nyumbani kwa familia yake kukiwa
na amani, sisi kupitia mkutano huu tuungane kuhakikisha Taifa letu linabaki
salama. Sekta ya habari ni nyenzo muhimu katika kulinda na kudumisha amani
katika kipindi chote cha uchaguzi,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa
kutokana na mazingira wezeshi kwa sekta hiyo ya habari Tanzania kwa sasa ina
idadi kubwa ya vyombo vya habari ikilinganishwa na miaka iliyopita, ambapo kuna
jumla ya magazeti 375, vituo vya redio 247, vyombo vya habari vya mtandaoni
355, blogs 72 na vituo vya televisheni 68, hivyo amevitaka vyombo hivyo
kukumbushana wajibu wao na kuzingatia miiko na maadili ya taaluma yao na
kuilinda tasnia yao kwa wivu mkubwa.
Aidha, amesema kuwa
Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha Sekta ya Habari na Utangazaji
nchini inakua na kutoa huduma bora kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ambapo
Aprili 6, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan alitoa maelekezo ya kuvifungulia vyombo vya habari vilivyokuwa
vimefungiwa. Na pia kuvirejeshea leseni vyombo vya habari ambavyo vilikuwa
vimemaliza adhabu zake ili viendelee na majukumu ya kuhabarisha jamii.
Amesema ni hatua
ambayo inadhihirisha kuwa Serikali ya
Dkt. Samia inaendeleza dhana ya kuheshimu na kuipa kipaumbele sekta ya habari
nchini ili Watanzania wapate habari sahihi. Serikali itaendelea kuthamini na
kuenzi mchango wa sekta ya habari, aidha, katika kutekeleza kwa vitendo falsafa
ya "4Rs" yaani Maridhiano (Reconciliation), Ustahimilivu
(Resilience), Mageuzi (Reforms), na Ujenzi Mpya wa Taifa(Rebuilding) bado sekta
ya habari inahitajika na mchango wake ni
wa muhimu.
Hatahivyo, Dkt.
Biteko amesema kutokana na matumizi makubwa ya teknolojia na mitandao ya
kijamii sekta ya habari ina jukumu kubwa la kupambana na taarifa potofu na
kuhakikisha kuwa jamii inapata taarifa sahihi kwa njia ya kidigitali kwa
kutumia lugha ya staha, kuepuka uchochezi na kuripoti kwa usawa, vyombo vya
habari huchangia katika kudumisha utulivu wa kitaifa.
Fauka ya hayo,
ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi wanayoifanya kuandaa
uchaguzi wa mwaka 2025 na kusema kuwa ni Rais Samia angependa kuona uchaguzi
unafanyika kwa haki na amani.
“ Ni matarajio yetu
kuwa Tume itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kwa karibu, kuhakikisha
wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu taratibu zote za uchaguzi. Ushirikiano
huu ni nguzo muhimu ya kuimarisha imani ya wananchi kwa mchakato wa uchaguzi,”
amemalizia Dkt. Biteko.
Kwa upande wake,
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi amesema
kuwa kupitia mkutano huo wa wadau wa
sekta ya habari wanalenga kuweka msingi madhubuti wa ushirikiano kati ya
Serikali, vyombo vya habari, asasi za kiraia, taasisi za usalama na taasisi
huru kama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ili kulinda amani, kuhimiza usawa wa
fursa kwa vyama vyote vya siasa, na kuruhusu wananchi kupata taarifa za msingi
zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuchagua viongozi
wao.
“Tunafahamu kuwa
uchaguzi ni tukio nyeti. Ni kipindi ambacho jamii inakuwa na matarajio makubwa
ya kupata taarifa zilizo sahihi, kwa wakati na zisizo na upendeleo. Ndiyo maana
mkutano huu pia umehusisha vyombo vya ulinzi na usalama, ili kwa pamoja
tuhakikishe kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira salama,
bila vitisho wala bugudha. Ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi na vyombo vya
habari ni jambo la msingi na tunalipa kipaumbele katika mjadala wetu wa leo,”
amesema Prof. Kabudi.
Naye, Mkuu wa Wilaya
ya Ubungo, Mhe. Albert Msando akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema wataendelea kushirikiana na vyombo vya
habari ili kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kutoka ndani ya Mkoa huo na
Wilaya zake ili kuhabarisha wananchi.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson
Msigwa amesema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wameona umuhimu wa kuungana katika mkutano huo
kwa lengo la kujadiliana ili kuhakikisha sekta ya habari inashiriki Uchaguzi Mkuu kwa mwaka 2025 kwa
weledi.
“Mwaka huu
tunashiriki Uchaguzi Mkuu tukiwa tumesimamia weledi, tumeanza kuendesha taaluma
yetu kitaalamu na sasa tuna mfumo wa kidigiti wa kusajili na kutoa ithibati kwa
waandishi wa habari,” amesema Msigwa.
Pamoja na ufunguzi wa
mkutano huo, Dkt. Biteko amezindua rasmi Mfumo wa Kidigiti wa TAI – Habari wa
kusajili na kutoa ithibati kwa waandishi wa habari ambao unasimamiwa na Bodi ya
Ithibati ya Waandishi wa Habari ambapo hadi
sasa Bodi hiyo imesajili waandishi wa habari zaidi ya 2900 kupitia mfumo
huo ambao unachakata taarifa zote muhimu
za mwandishi wa habari na kisha kumpatia mwandishi wa habari kitambulisho cha
kidigiti yaani Digital Press Card.
Na. Ofisi ya Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni