Mamlaka ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama, imefanikiwa kukamata jumla ya kilo 37,197.142 za dawa za
kulevya katika operesheni zilizofanyika maeneo mbalimbali nchini kati ya Mei
hadi Julai 2025.
Katika taarifa
iliyotolewa leo na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Mamlaka hiyo, dawa
hizo ni pamoja na kilo 11,031.42 za Mitragyna Speciosa (aina ya dawa mpya za
kulevya), bangi kilo 24,873.56, mirungi kilo 1,274.47, skanka kilo 13.42,
heroin kilo 2.21 na methamphetamine gramu 1.42.
Aidha, dawa za tiba
zenye asili ya kulevya zilizokamatwa ni pamoja na ketamine kilo 1.92 na vidonge
1,000 vya flunitrazepam (maarufu kama rohypnol). Pia, zilikamatwa lita 6 za
kemikali bashirifu aina ya hydrochloric acid.
Katika operesheni
hiyo, ekari 1,045.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika mikoa mbalimbali
ikiwemo Ruvuma, Mbeya, Mara, Kagera, Dodoma, Tabora, Morogoro na Arusha.
Shehena Kutoka Sri Lanka Yakamatwa Temeke
Katika operesheni
maalum iliyofanyika kwenye bandari kavu ya Temeke, Dar es Salaam, zilikamatwa
kilo 11,031.42 za Mitragyna Speciosa zilizokuwa zimeingizwa nchini kutoka Sri
Lanka, zikiwa zimefungwa kwenye maboksi yenye nembo ya mbolea. Mmea huu,
unaojulikana pia kama Kratom, una kemikali zinazojulikana kwa majina ya
Mitragynine na 7-Hydroxymitragynine, ambazo huathiri mfumo wa fahamu,
husababisha uraibu na hata vifo vya ghafla.
Watuhumiwa 64 Wakamatwa
Katika operesheni
hiyo ya kitaifa, jumla ya watuhumiwa 64 walikamatwa wakihusishwa moja kwa moja
na usambazaji au umiliki wa dawa hizo.
Katika tukio jingine
jijini Dar es Salaam, eneo la Posta, watuhumiwa sita waliokamatwa walijumuisha
raia wawili wa China waliotajwa kwa majina ya Chein Bai na Qixian Xin.
Walikutwa na methamphetamine gramu 1.42, vidonge 1,000 vya rohypnol, na
ketamine kilo 1.92.
Kiwanda Bubu cha Biskuti za Bangi
Katika eneo la Sinza,
jijini Dar es Salaam, watu wawili walikamatwa wakiwa wamiliki wa kiwanda bubu
kilichokuwa kikitengeneza biskuti zilizochanganywa na bangi na kuzisambaza
katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara. Mkoani Lindi, mfanyabiashara
wa madini naye alikamatwa akisambaza biskuti zenye bangi.
Heroin Kutoka Msumbiji Yazuiwa
Katika hatua
nyingine, kilo 26 za heroin zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Msumbiji kuelekea
Tanzania zilizuiawa kabla ya kuingia nchini.
Maiti Zaanza Kutumiwa Kusafirisha Dawa
DCEA pia imebaini
kuwa baadhi ya magenge ya kihalifu yamerudi kutumia mbinu hatarishi za
kusafirisha dawa za kulevya kwa kutumia maiti za binadamu, maarufu kama
"begi".
Aidha, mamlaka hiyo
imeonya kuwa raia wa kigeni wamekuwa wakiwatumia Watanzania kusafirisha au
kusambaza dawa za kulevya kwa njia ya mahusiano ya kirafiki, kisha kuwatumia
katika kampuni, usafiri wa bodaboda, bajaji, teksi na hata kupitia wasambazaji
wa vifurushi.
Mamlaka Yaonya Umma
DCEA imewataka
wananchi kuwa waangalifu na mizigo wanayotumwa au wanayopokea, hasa kutoka kwa
watu wasiowafahamu vyema, ili kuepuka kuingizwa katika biashara hiyo haramu.
Mamlaka hiyo
imewataka Watanzania kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa
taarifa za wale wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, huku
ikiahidi kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kuhusika.

0 Maoni