Polisi wawili washikiliwa kumuua kwa kumpiga risasi mkazi wa Dodoma

 

Polisi wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa tuhuma za kuhusika katika tukio la kumpiga risasi na kusababisha kifo cha Frank Sanga (32), mkazi wa Kitongoji cha Mgomwa, Kata ya Matumbulu, jijini Dodoma.

Tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kutokea Julai 19, 2025, majira ya saa 7:30 mchana katika maeneo ya Matumbulu, wakati marehemu Frank alipojaribu kumsaidia ndugu yake aliyekuwa amekamatwa na askari hao kwa makosa ya usalama barabarani, kwa lengo la kuzuia asipelekwe kituoni.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa leo Julai 21, 2025, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, askari hao walimkamata mwendesha pikipiki (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi) kwa makosa ya kutokuwa na leseni, kutokuvaa kofia ngumu, na kuendesha chombo kibovu.

Kamanda Hyera amesema baada ya kukamatwa, dereva huyo alipiga simu kwa ndugu zake ambao walifika kwa wingi wakiwa kwenye pikipiki tano, kila moja ikiwa na watu zaidi ya wawili, na kujaribu kwa nguvu kuichukua pikipiki hiyo na kumwachia huru ndugu yao.

“Katika hali hiyo ya vurugu na kuonekana kama walikuwa wamejipanga kupambana na askari, askari walilazimika kujihami kwa kufyatua risasi, ambapo Frank Sanga alijeruhiwa kwenye paja na ugoko wa mguu wa kushoto. Alikimbizwa hospitalini kwa matibabu lakini alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa huduma,” amesema Kamanda Hyera.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi limechukua hatua za awali kwa kuwasimamisha kazi askari hao na kuwashikilia kwa uchunguzi zaidi, huku likiahidi kuchukua hatua stahiki endapo watabainika kuwa walikiuka maadili ya kazi zao.

Tukio hili limezua taharuki kwa wakazi wa Matumbulu, huku baadhi wakitaka uchunguzi huru kufanyika na haki kutendeka kwa familia ya marehemu.

Chapisha Maoni

0 Maoni