Hospitali ya Taifa
Muhimbili-Mloganzila imeanza kambi maalum ya kutengeneza mishipa ya kuchuja
damu sambamba na kupandikiza figo kwa wagonjwa wenye changamoto za figo ambayo
itahitimishwa rasmi Julai 23, 2025.
Kambi hiyo inafanywa na
wataalam wa Muhimbili Mloganzila kwa kushirikiana na jopo la wataalam kutoka
Korea Kusini linalo ongozwa na Prof. Park Kwan Tae ambaye ni Daktari Bingwa
Bobezi wa Upasuaji chini ya uaratibu wa Taasisi ya Africa Future Foundation
(AFF) ya nchini Korea Kusini.
Upandikizaji wa figo
unafanyika kwa kuvuna figo kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia matundu madogo
(Laparascopic Hand Assisted Donor Nephroctomy) utaalam ambao kwa hapa nchini
unapatikana Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila pekee.
Aidha,wataalam mbalimbali
kutoka ndani na nje ya nchi wanajengewa uwezo wa kutoa huduma hizo katika
maeneo yao ili kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kwenda mbali na maeneo yao
kufuata huduma hizo.
Hadi kuhitimishwa kwa
kambi hiyo wananchi takribani 60 watanufaika na huduma za kutengenezewa mishipa
ya kuchuja damu na wananchi wanne watapandikizwa figo na kufikisha idadi ya wanufaika
waliopandikizwa figo kufikia 19 tangu huduma hizo zilipoanza rasmi katika
hospitali hiyo mwaka 2023.
0 Maoni