Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameonesha kuguswa na kushtushwa na tukio la kusikitisha linalomuhusisha mama aitwaye Mary Mushi (26), mkazi wa Kata ya Masama Kusini, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, anayedaiwa kuwaua watoto wake wawili wa kike kwa kuwachoma visu tumboni, kabla ya yeye mwenyewe kujijeruhi kwenye koromeo.
Kwa mujibu wa taarifa
zilizothibitishwa na vyombo vya usalama, chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa
ni msongo wa mawazo unaotokana na mgogoro wa kimapenzi (mchepuko). Mary
aliripotiwa kufanya tukio hilo na kisha kujaribu kujiua kwa kujichoma na kisu
hicho hicho.
Akizungumzia tukio
hilo, Mhe. Gwajima amesema:
“Jamani jamani,
hasira gani hizi? Akili gani hizi? Wanawake, inabidi tuwe na mazungumzo ya
kina. Mambo haya yanatisha, hayana tija hapa duniani wala kwa maisha ya baadae.
Inawezekana kuushinda msongo wa mawazo na kusonga mbele kama mshindi.”
Waziri Gwajima
amewahimiza wanawake na jamii kwa ujumla kutafuta msaada wa kisaikolojia pale
wanapokumbwa na changamoto za kiakili, akisisitiza kuwa huduma za ustawi wa
jamii zipo kwa ajili ya kusaidia.
“Kama kuna mwingine
anayepitia msongo wa mawazo, tafadhali jamani, wafikishieni habari kwamba
ustawi wa jamii tupo kwa ajili yao. Tutawasaidia kuibuka washindi wakiwa na
tabasamu la haki. Mimi mwenyewe, napatikana – sms njoo 0765 345 777. Linda uhai
wako na wa mwingine,” aliongeza Waziri Gwajima.
Miili ya watoto hao
wawili ilizikwa Juni 24, 2025 katika makaburi ya wilayani Hai. Wakati huo huo,
mama huyo anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC
akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi wakati uchunguzi wa kina ukiendelea.
Tukio hili limeibua
hisia kali mitandaoni na kwa wananchi wa maeneo ya jirani, huku wito ukitolewa
kwa jamii kuwa na tahadhari na kutoa msaada wa kisaikolojia kwa wanaoonyesha
dalili za matatizo ya afya ya akili.
0 Maoni