Serikali imependekeza
kufanya marekebisho ya Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya eneo
la Ngorongoro (NCAA), Sura 284, kwa lengo la kubadilisha mgawanyo wa mapato
yatokanayo na huduma zinazotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania
(TANAPA).
Waziri wa Fedha, Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa pendekezo hilo Bungeni leo alipowasilisha
Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali kupitia Sheria ya Fedha ya
mwaka 2025, mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloendelea
jijini Dodoma.
Kupitia marekebisho
hayo, Serikali inapendekeza kufuta kifungu kidogo cha (b) kilichokuwa kinaitaka
mgao wa asilimia 91 ya mapato kuwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Badala yake, sasa mapato
yatokanayo na huduma zinazotolewa TANAPA asilimia 51 itawekwa katika akaunti iliyopo
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na matumizi yake yatahitaji kibali kutoka kwa
Mlipaji Mkuu wa Serikali.
Aidha, asilimia 40 ya
mapato hayo itaendelea kupelekwa moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Mabadiliko haya
yanakuja wakati kukiwa na mjadala mpana kuhusu mustakabali wa eneo la Ngorongoro,
ambalo ni urithi wa dunia unaokabiliwa na changamoto za kiikolojia na kijamii
kutokana na shughuli za binadamu na ongezeko la watu.
Wadau wa uhifadhi,
haki za jamii na maendeleo wameelezea matumaini kuwa mfumo huu mpya wa mgao wa
mapato utasaidia kuboresha utendaji wa NCAA bila kuathiri mchango wake kwa
Serikali Kuu.
0 Maoni