Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja.
Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko leo Juni 24,2025, jijini Dar es Salaam
amewatunuku vyeti vya pongezi wanamichezo (14) waliofanya vizuri kwenye michezo
ya riadha (2) na mchezo wa kuvuta kamba (12) katika Mashindano ya Shirikisho la
Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA)
yaliyofanyika mnamo mwezi Novemba 2024.
Akizungumza wakati wa
utoaji wa vyeti hivyo, Mej.Jen (Mstaafu) Semfuko amesema michezo ni miongoni mwa nyenzo kubwa
katika kuongeza mshikamano kwenye Majeshi.
" Kazi kubwa ya
michezo katika majeshi ni kuunganisha jeshi kwa pamoja, kwa lugha ya kigeni
tunasema esprit de corps," amesema
Semfuko.
Kadhalika, Mej. Jen
(Mstaafu) Semfuko amewapongeza wanamichezo hao kwa kushinda Medali na Kombe na
akasisitiza kuwa Bodi ya Wakurugenzi itahakikisha wanamichezo wanaendelea kupata motisha mbalimbali ili
kuongeza morali ya ushindi katika mashindano
ambayo TAWA ni mshiriki.
" Menejimenti
itafanya bidii, ili kuhakikisha tunashinda michezo mingine na kwa kuanza, Bodi
inatoa zawadi hii ndogo kwenu nyote kwa kutuletea ushindi huu," amesema
Semfuko.
Sambamba na hilo,
Semfuko amewataka wanamichezo hao kuwa mfano kwa watumishi wengine kwa
kuwahamasisha ili washiriki katika michezo mbalimbali.
Awali, akimkaribisha
Mej. Jen (Mstaafu) Semfuko, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Kabange
amesema TAWA inashiriki kwenye mashindano ya michezo mbalimbali kwa lengo la
kutangaza vivutio vya utalii vinavyosimamiwa na TAWA, kuimarisha afya za Askari
na kuimarisha mahusiano kati ya TAWA na Taasisi zingine.
Aidha, Kamishna
Kabange ameongeza kuwa katika Mashindano ya mwaka huu Menejimenti imejipanga
vizuri ili kuhakikisha vikosi vya TAWA
vinakuwa bora na kujiweka katika nafasi ya ushindi zaidi.
Naye , Mratibu wa
michezo - TAWA, Carlos Mbiro ameishukuru Bodi ya Wakurugenzi kwa kuwatunuku
zawadi hizo na akasema kama wanamichezo wanafarijika sana na wanaahidi
kuendelea kufanya vizuri katika mashindano mengine yatakayofanyika.
Na. Joyce Ndunguru - Dar es Salaam
0 Maoni