Katibu Mkuu wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa maoni
yoyote yanayolenga kuhakikisha Tanzania inaendelea kudumisha amani na utulivu,
hayajawahi kupuuzwa na hayatapuuzwa.
Aidha, Balozi Nchimbi
amemwelezea Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ni kiongozi mwanamke ambaye uongozi wake,
umeongeza heshima kubwa kwa wanawake na Tanzania, akiendeleza safari
iliyoanzishwa na viongozi wengine wanawake jasiri, tangu wakati wa kudai uhuru
na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia.
Balozi Dkt. Nchimbi
amesema hayo alipokuwa akifungua Jukwaa la Wanawake wa Arusha 2025,
lililowakutanisha wanawake katika kujadili maada ya ‘Safari ya Mwanamke Arusha
2025’, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini Arusha,
Jumanne, tarehe 24 Juni 2025.
“Hivyo ndivyo
wanawake wanalitazama taifa letu (kama wanavyotazama watoto wao). Wanataka nchi
yetu iendelee kuwa na amani, nchi yetu iendelee kuwa tulivu. Nataka nitumie
nafasi hii, kuwahakikishia wanawake wa Tanzania, kwamba CCM inatambua dhamana
yake ya kulinda amani ya nchi yetu.”
“Nataka
niwahakikishie viongozi wa mila, viongozi wa dini, viongozi wa taasisi za
kijamii, niwahakikishie Watanzania wote, kwamba maoni yenu yanayohusu
kuendeleza amani na utulivu katika nchi yetu, hatujawahi kuyapuuza kama Chama
Cha Mapinduzi,” alisema Balozi Nchimbi na kuongeza;
“Na tukitambua kuwa
amani ndiyo kipaumbele cha kwanza cha mwanamke wa Tanzania…akitambua kwamba
kuilinda amani ni kuilinda nchi yetu, kukilinda kizazi cha sasa na kizazi
kijacho, tutaendelea kuisimamia amani ya nchi yetu kwa nguvu zetu zote.”
Jukwaa hilo ambalo
wazungumzaji wakuu wa mada hiyo walikuwa ni pamoja na Mama Fatma Karume, mjane
wa Hayati Mzee Abeid Amani Karume, Mama Anne Makinda, Dkt. Asha-rose Migiro,
Bi. Zakhia Meghji, na wanawake wengine vijana, lililenga kuzungumzia safari ya
mwanamke katika nyanja mbalimbali za maisha, kisiasa, kiuchumi na
kijamii nchini.
0 Maoni