Rais Dkt. Samia aipongeza JKCI kwa kuwafuata wananchi mahali walipo

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa juhudi zake za kuwafuata wananchi popote walipo na kuwapatia huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo bila malipo.

Rais Dkt. Samia alitoa pongezi hizo jana katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwa Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Rais alisema taasisi zinazotoa huduma zenye manufaa kwa jamii zinastahili kutambuliwa na kupongezwa, kama ambavyo JKCI imekuwa ikifanya kupitia huduma zake za tiba mkoba.

"Taasisi ambazo zinatoa mchango wao kwa jamii kutokana na huduma wanazotoa nazo zinatakiwa kuonekana na kuonesha wanachangia kiasi gani kwa umma. JKCI wamekuwa mstari wa mbele na huduma yao inagusa wananchi moja kwa moja," alisema Rais Dkt. Samia.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema JKCI imefanikiwa kutoa gawio la Shilingi Bilioni 2 kupitia huduma za moyo zilizotolewa kwa wananchi 27,600 katika mikoa 16 nchini kupitia kambi maalum ya Tiba Mkoba ya Mhe. Rais Samia.

"JKCI hata tusipowaona kwenye makusanyo ya fedha, tunaona matokeo yao kwenye maisha ya watu. Huduma ya tiba mkoba imefika mikoa 16 na kuwanufaisha maelfu ya Watanzania," alisema Mchechu.

Aidha, Mchechu alibainisha kuwa kwa mara ya kwanza JKCI imeweza kupanua wigo wa huduma zake kwa kuanzisha kliniki nje ya makao makuu, hatua inayodhihirisha ukuaji na mafanikio ya taasisi hiyo.

“Sasa hivi ukihitaji huduma za JKCI, unaweza kuzifuata katika matawi yao yaliyopo Oysterbay, Kawe, Dar Group Hospitali, na Arusha AICC,” aliongeza.

Msajili huyo alisisitiza kuwa ofisi yake itaendelea kufuatilia namna mafanikio ya taasisi kama JKCI yanavyoweza kuwagusa moja kwa moja watendaji wake ili kuongeza ufanisi na kuchochea uwajibikaji zaidi katika utumishi wa umma.

Chapisha Maoni

0 Maoni