Waongoza utalii
kutoka kampuni mbalimbali zinazojihusisha na shughuli za utalii nchini
wameipongeza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa juhudi
wanazofanya kuboresha miundombinu ya
barabara katika Eneo la Hifadhi ya
Ngorongoro.
Wadau hao wameelezeq
hatua hiyo kuwa ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto zilizokuwa
zikiwakabili, hasa wakati wa msimu wa kilele cha utalii (high season).
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti katika geti la kuingia hifadhi ya Ngorongoro Juni 11, 2025,
baadhi waongoza utalii hao wameeleza kuwa maboresho hayo yameleta mabadiliko
makubwa katika usafiri, kupunguza muda wa safari, kuongeza usalama wa wageni,
na kuboresha hali ya utalii katika hifadhi hiyo maarufu duniani.
“Tunatoa pongezi kwa
NCAA kwa kazi kubwa waliyoifanya kuboresha barabara, kwa sasa imekuwa rahisi zaidi kuwafikisha
wageni kwa haraka na salama kwenye maeneo ya vivutio vya utalii vilivyopo
Ngorongoro,” alisema Mohammed Tenga kutoka kumpuni ya Zara Tours.
Kwa upande wake
Walter Temba kutoka kampuni ya utalii ya Serengeti Smiles alieleza kuwa
maboresho ya miundombinu ya barabara yanayoendelea yamekuja kwa wakati muafaka,
ikizingatiwa kuwa sekta ya utalii nchini inaendelea kukua kwa kasi huku idadi
ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi ikiendelea kuongezeka kila mwaka.
“Kwa muda mrefu
tumekuwa tukikumbana na changamoto kubwa hasa wakati wa mvua magari yanakwama
na wageni kuharibika hata kabla ya kufika kwenye vivutio. Lakini sasa hali ni
tofauti kabisa, barabara zimekarabatiwa kwa kiwango kizuri na zinaweza kupitika
hata kipindi cha mvua ombi letu ni kuwa jitihada hizi ziwe endelevu,” alisema
Temba.
Kwa Mujibu wa NCAA,
maboresho ya barabara ni sehemu ya maandalizi ya taasisi hiyo kukabiliana na
ongezeko kubwa la watalii ambalo limeanza mwezi juni ambalo linatarajiwa
kuongezeka hadi mwezi Oktoba kila
mwaka.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hupokea maelfu
ya wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani wanaokuja kutembelea vivutio vya
utalii ambapo takwimu zinaonesha kuwa kati ya Mwezi Julai 2024 hadi Mei, 2025
jumla ya watalii 972,896 wametembelea hifadhi kwa shughuli za utalii.
Na. Mwandishi wa NCAA
- Ngorongoro
0 Maoni