Elon Musk ajutia kamshambulia Rais Donald Trump

 

Bilionea Elon Musk amesema anajutia baadhi ya kauli alizozitoa dhidi ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kufuatia mvutano wao wa maneno uliotokea kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita.

Kupitia mtandao wake wa kijamii, X (zamani Twitter), Musk aliandika:

"Ninajutia baadhi ya machapisho yangu kuhusu Rais Donald Trump wiki iliyopita. Nilikwenda mbali kupita kiasi." 

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya mvutano wao kufikia kilele, ambapo mmiliki huyo wa kampuni ya Tesla aliuita muswada wa rais Trump kuwa “aibu na wa kuchukiza” maneno yaliyosababisha mvutano mkubwa wa kisiasa.

Rais Trump, kwa upande wake, alijibu vikali kwa kusema kuwa uhusiano wake na Musk umefikia kikomo na hana mpango wowote wa kuurekebisha.

Kabla ya mvutano huo, Musk alikuwa miongoni mwa wafadhili wakubwa wa kampeni ya Trump ya kugombea urais mwaka 2024, na alikuwa akionekana kama mshirika wake wa karibu kisiasa.

Katika hatua nyingine kali, aliyekuwa mshauri wa Trump, Steve Bannon, alimtaka Musk, ambaye ni mzaliwa wa Afrika Kusini, arejeshwe nchini kwake akidai amekuwa "tisho kwa usalama wa taifa".

Chapisha Maoni

0 Maoni