Makamu Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema kaulimbiu ya
"Mitano Tena" ni kwa ajili ya mgombea urais wa chama hicho Dk. Samia
Suluhu Hassan na mgombea mwenza wake Dk. Emmanuel Nchimbi pekee, huku akiweka
wazi kuwa wabunge na madiwani hawajapewa uhakika bali watapitia mchujo wa ndani
ya chama.
Wasira ameyasema hayo
leo Juni 11, 2025, alipokuwa akizungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa
CCM wa Wilaya ya Nyasa, kilichofanyika katika mji wa Mbamba Bay mkoani Ruvuma,
ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuimarisha Chama.
“Niwaambie wana CCM
wenzangu, tunaposema Mitano Tena ni kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na mgombea
mwenza wake Dk. Emmanuel Nchimbi. Kwa wabunge na madiwani tusubiri mchujo ndani
ya Chama,” alisema Wasira huku akisisitiza kuwa mchujo huo utafanyika kwa haki
na kwa kuzingatia maoni ya wananchi.
Ameongeza kuwa mwaka
huu CCM imeongeza idadi ya wapigakura wa maoni katika maeneo mbalimbali nchini
ili kuhakikisha mchakato wa kupata wagombea unakuwa shirikishi zaidi.
“Kwa mfano hapa
Nyasa, mwaka uliopita walikuwa wapigakura 900, sasa hivi wako 1,300. Hii ni
ishara ya kupanua demokrasia ndani ya Chama,” alifafanua.
Wasira amesisitiza
kuwa si kila kiongozi aliyepo madarakani atapewa fursa ya kurejea moja kwa
moja, bali ni wananchi kupitia kura za maoni ndio watakaoamua nani anafaa kuendelea.
“Sio kila mtu ni
Mitano Tena, bali ni kwa Rais Samia. Wengine tutachujana. Mbunge au diwani
anayetaka kuendelea, anatakiwa akubali kupimwa na wapigakura wa kata yake,”
alieleza.
Katika kikao hicho,
alionya dhidi ya wagombea wanaotafuta uongozi kwa kutumia fedha kununua kura,
akisema chama kinataka watu safi na wanaokubalika mbele ya wananchi.
“Mabalozi wa CCM wana
jukumu la kuhakikisha wanapitisha majina ya wagombea ambao wanauzika kwa
wananchi, si wale waliopita kwa hela. Heshima ya mjumbe ni kusikiliza sauti ya
waliomchagua,” alisema.
Katika ziara hiyo,
Wasira pia alikagua maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay, wilayani
Nyasa, mradi ambao Serikali imewekeza fedha kwa ajili ya kuuboresha na
kuimarisha miundombinu ya usafirishaji katika Ukanda wa Ziwa Nyasa.
0 Maoni