Katibu Mkuu wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Dkt. Charles Kitima ameongoza
Adhimisho la Misa Takatifu ya shukrani kwa mara ya kwanza baada ya kutoka
hospitali alikokuwa anapatiwa matibabu kwa takribani mwezi mmoja baada ya tukio
la shambulizi dhidi yake.
Padri Kitima
ameongoza adhimisho hilo katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
lililopo TEC-Kurasini, Dar es salaam leo Juni 3, 2024 pamoja na mapadri, watawa
na wafanyakazi wengine wa Sekretarieti ya TEC, kwa nia ya kumshukuru Mungu kwa
kumponya.
Akitoa homilia katika
adhimisho hilo Padri Kitima amemshukuru Mungu kwa kumponya dhidi ya shambulizi
lililolenga kukatisha uhai wake, huku pia akiwashukuru watu wote kwa sala na
matashi mema katika kipindi chote cha matibabu yake.
“Tunamshukuru Mungu
kwa wema wake, pia tunawashukuru watu wote walioguswa na tukio lile. Tuombe ili
Kanisa lizidi kuwa imara siku zote bila kutetereka. Tukumbuke kuwa Kanisa
Katoliki ni taasisi inayotegemewa na watu wengi, ni sauti ya watu wasio na
sauti, ni msindikizaji wa wanyonge. Tuliombee Kanisa letu lizidi kuwa mwanga na
matumaini ya Watanzania” ameeleza Padri Kitima.
Aidha, Padri Kitima
amewataka wana Sekreatarieti ya TEC kuyapokea mambo yote yaliyotokea kwa jicho
na moyo wa imani akisisitiza kuwa katika mambo yote ambayo Kanisa linayasimamia
kwa ajili ya wanyonge, Mungu atayasikiliza.
“Mungu hatakaa kimya,
atajibu sala zetu. Tuwe imara katika kazi zetu, tukumbuke kuwa hata mitume
walipata misukosuko. Tusirudi nyuma, tubaki katika imani
thabiti,” ameongeza.
Na. Pascal Mwanache -
TEC
0 Maoni